• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Viwanda vya unga vyafungwa kufuatia ukosefu wa mahindi

Viwanda vya unga vyafungwa kufuatia ukosefu wa mahindi

Na BARNABAS BII

VIWANDA vya kusaga unga wa mahindi katika maeneo la Magharibi na Kati vimesitisha shughuli kutokana na ukosefu wa mahindi.

Hii inatokana na hatua ya serikali kuchelewa kutoa magunia milioni 2 ili kukabiliana na makali ya njaa nchini.

Tayari viwanda 10 vimefungwa kwa muda na wafanyakazi kuagizwa kwenda likizo ya lazima kutokana na ukosefu wa mahindi.

“Hatujakuwa tukipata mahindi ya kutosha sasa tumeamua kufunga viwanda,” akasema msimamizi wa moja ya viwanda vilivyoathiriwa.

Alisema karibu asilimia 80 ya viwanda vimesitisha operesheni kutokana na uhaba wa mahindi.

Viwanda vilivyoathiriwa zaidi viko katika maeneo ya Bungoma, Busia, Kisumu, Narok, Kajiado na vingine vinne katika eneo la Kati.

Uhaba wa mahindi umesababisha kuongezeka kwa bei ya unga na umesababisha na ukame ulioshuhudiwa miezi michache iliyopita.

“Viwanda vilivyoko katika maeneo ya Eldoret, Moi’s Bride na Kitale bado vingali na mahindi lakini yataisha ndani ya miezi miwili,” akasema Bw David Kosgei, msimamizi wa kiwanda cha nafaka mjini Eldoret.

Viwanda vitano; Mombasa Millers, Unga, Pembe, Dolar na Kitui Millers vimesalia na mahindi yatakayodumu kwa wiki mbili tu.

Serikali ilikuwa imeahidi kutoa magunia milioni mbili ili kukinga Wakenya dhidi ya bei ya unga wa mahindi ambayo inazidi kupanda. Kilo mbili za unga wa mahindi zinauzwa wka kati ya Sh115 na Sh130 ikilinganishwa na Sh80 wiki chache zilizopita.

Bei ya gunia moja la kilo 90 imepanda kutoka Sh2,600 hadi Sh3,200 katika eneo la North Rift.

Kulingana na waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri, viwanda vya kusaga nafaka vilifaa kuuziwa jumla ya magunia milioni mbili kwa kati ya Sh2,500 na Sh3,000.

Lakini watumiaji wa unga wa mahindi sasa wanataka waziri kuelezea Wakenya kiwango cha magunia ya mahindi yanayohifadhiwa katika Hifadhi ya Mazao na Nafaka (NCPB).

Watumiaji pia wamehimiza serikali kuchukua hatua za haraka kunusuru zaidi ya Wakenya milioni 2.2 wanaokabiliwa na makali ya njaa.

“Waziri anafaa kujitokeza na kuwaeleza Wakenya kiasi cha mahindi yaliyosalia. Hatuwezi kuendelea na mchezo wa pata potea na maisha ya Wakenya,” akasema James Maina, mfanyabiashara mjini Eldoret.

Serikali imeshikilia kuwa haitaagiza mahindi kutoka mataifa ya kigeni.

You can share this post!

Pendekezo wanaochanga zaidi ya Sh100,000 waripoti kwa EACC

Vijana wamekataa kuwekeza kwa hazina ya uzeeni –...

adminleo