Vijana wamekataa kuwekeza kwa hazina ya uzeeni – Ripoti
Na LEONARD ONYANGO
IDADI kubwa ya vijana nchini hawawekezi katika hazina za malipo ya uzeeni, ripoti imefichua.
Kulingana na ripoti ya utafiti wa Infotrak idadi ya Wakenya wanaowekeza katika hazina za pensheni za uzeeni imepungua hadi asilimia 10.
Utafiti huo, ulibaini kuwa badala ya kuwekeza katika hazina ya malipo ya uzeeni, baadhi ya Wakenya sasa wameamua wawe wanawekeza katika mali kama vile mashamba na biashara nyinginezo zitakazowawezesha kujipatia hela uzeeni wakati watakapostaafu.
Akizungumza wakati wa kutolewa kwa ripoti ya utafiti huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Hazina ya Pensheni ya Kaunti (CPF) Hosea Kili, alisema kuna hatari ya Wakenya wengi kuteseka baada ya kustaafu kutokana na ukosefu wa malipo ya pensheni.
“Idadi kubwa ya vijana wanaofanya kazi hawawekezi katika hazina za malipo ya uzeeni. Hiyo inamaanisha kwamba watapata taabu watakapostaafu kwani hawataweza kujikimu kimaisha,” akasema Bw Kili.
Ripoti hiyo ilitolewa wakati wa maadhimisho ya miaka 90 tangu kuanzishwa kwa Hazina ya Pensheni ya Serikali za Mitaa (Laptrust) jijini Nairobi.
“Inasikitisha kwamba asilimia 90 ya Wakenya hawawekezi katika hazina zitakazowafaa baada ya kustaafu,” akasema Bw Kili.
Mkurugenzi Mtendaji wa Infotrak, Angela Ambitho, alisema utafiti huo ulifadhiliwa na CPF na ulifanywa kati ya kaya 1,500 kote nchini.
Bi Ambitho alisema kuwa kupungua kwa idadi ya watu wanaowekeza katika hazina za malipo ya uzeeni ni ishara kwamba vijana wanahitji elimu kuhusu umuhimu wa kuwekeza kwa ajili ya maisha ya baada ya kustaafu.
Hazina ya ilianzishwa mnamo 1929 kwa ajili ya kuwalipa pensheni wafanyakazi waliohudumu katika serikali ya mkoloni.
Jumla ya wafanyakazi 20,074 wa serikali ya kitaifa na kaunti zote 47 wanawekeza katika hazina ya Laptrust na watu 7,098 wanapokea malipo ya uzeeni.