TAHARIRI: Watu wasitie siasa zenye ukabila KNH
Na MHARIRI
SHINIKIZO la kumtaka Waziri wa Afya Sicily Kariuki aondoke kwa kumpa afisa mkuu wa Hospitali Kuu ya Kenyatta likizo ya lazima, ni jambo linalostahili kushtumiwa vikali.
Waziri alichukua hatua hiyo ili kutoa nafasi ya uchunguzi kufanywa katika hospitali hiyo, ambayo imegonga vichwa vya habari katika siku za hivi punde.
Huenda kweli kuna njama za kumuondoa afisa mkuu huyo, lakini pia lazima Wakenya wajue ukweli kuhusu yanayojiri katika hospitali hiyo, ndiposa hatua hiyo imechukuliwa.
Kwa hivyo, hatua ya baadhi ya viongozi kujitokeza kudai kusimama pamoja na mtu wa jamii yao, inastahili kushtumiwa. Lazima viongozi wawe wakitoa nafasi ya uchunguzi kufanywa ili ukweli ubainike.
Yafaa watambue kuwa kama afisa mkuu wa hospitali, Bi Koros alikuwa na wajibu wa kufuatilia kinachojiri, hata kama hakuwa mhusika binafsi.
Ni jambo la kushangaza jamii zinapojitokeza kutetea “mtu wao” bila ya kubainisha ukweli ikiwa wana makosa au la.
Kwa taifa hili kukabiliana na ukabila lazima watu waweze kuelewa kuwa hata watu wa jamii zao hufanya makosa, na wanapofanya makosa, lazima wachukuliwe hatua. Wakenya wanastahili kujifunza kutetea haki na sio kabila, kwa nchi hii kuweza kuimarika.
Ingawaje si vyema kukaa kimya mtu anapoona dhuluma, ni muhimu kuhakikisha kuwa unachotetea ni cha haki. Yashangaza kuwaona watu wa jamii fulani wakijitokeza kuwatetea maafisa wakuu serikalini ambao huenda wameshtumiwa kwa ufisadi, ilhali ni pesa za mlipaji kodi ambazo zimefujwa.
Katika suala hili la hospitali ya Kenyatta, tunataka kuona uchunguzi wa kina na Wakenya kuelezewa matokeo yake, bila kuingiza siasa ama dhuluma. Ikiwa afisa mkuu hana makosa yoyote, bila shaka Wakenya wanatarajia kuwa arejeshwe kazini.
Na iwapo ataondolewa, Wakenya pia wafafanuliwe sababu zinazoelekeza kuondolewa kwake.
Hata hivyo, kwa sasa tunatarajia kuwa sawa na jinsi ambavyo malalamishi haya yameshughulikiwa upesi, vile vile huduma katika hospitali hii zitaimarishwa, kuhakikisha mgao wa fedha unaotosha, kuwepo kwa vifaa pamoja na kuwajali wahudumu waliopo.
Serikali ihakikishe kuwa juhudi na hatua inazochukua sio za kuwafumba Wakenya macho kwa muda mfupi, na kesho tunasalia kuzungumzia masuala yale yale.