• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 2:13 PM
Shujaa juhudi ni kufuzu Olimpiki baada ya kunoa Raga ya Dunia

Shujaa juhudi ni kufuzu Olimpiki baada ya kunoa Raga ya Dunia

Na GEOFFREY ANENE

BAADA ya Raga ya Dunia ya msimu 2018-2019 kutamatika Jumapili, Kenya sasa inaelekeza macho kwa Kombe la Afrika litakaloandaliwa mjini Johannesburg nchini Afrika Kusini baadaye mwaka 2019 na kutumika kama mchujo wa Olimpiki mwaka 2020.

Vijana wa kocha Paul Murunga walitarajiwa kutua jijini Nairobi kutoka nchini Ufaransa Jumatatu usiku.

Watawania tiketi ya kuingia Olimpiki moja kwa moja dhidi ya mataifa 13. Nambari mbili na tatu wakishiriki mchujo mwingine wa dunia ili kufika jijini Tokyo mwaka ujao.

Shujaa ilimaliza makala ya kwanza ya raga ya wachezaji saba kila upande kwenye Olimpiki katika nafasi ya 11 kati ya mataifa 12 iliyoshiriki nchini Brazil mwaka 2016.

Itamenyana na Namibia, Zimbabwe, Zambia, Tunisia, Ghana, Morocco, Uganda, Botswana, Mauritius, Madagascar, Senegal, Ivory Coast na Nigeria hapo Novemba 8-9.

Kitakuwa kibarua kigumu katika mchujo huo kwa Shujaa isiposhughulikia maslahi ya wachezaji yaliyoifanya ikose huduma za wachezaji wazoefu kwa kipindi kirefu na kuponea tundu la sindano kutemwa kutoka Raga ya Dunia.

Mataifa ya Uganda, Zimbabwe na Namibia yamekuwa yakifanya vyema katika mashindano ya Afrika kwa hivyo Shujaa haitapata mtihani rahisi kufika Japan mwaka ujao.

Itakumbukwa kuwa Kenya ilipokonya Zimbabwe ushindi sekunde ya mwisho mwaka 2015 pale Dennis Ombachi aliifungia mguso kabla tu ya kipenga cha mwisho kulia na kuisaidia kushinda 19-17 na kuingia Olimpiki mwaka 2016.

Zimbabwe ni mabingwa watetezi wa Kombe la Afrika baada ya kulemea Kenya 17-5 mwaka jana. Wazimbabwe pia walishinda makala ya mwaka 2000 na 2012.

Uganda walitwaa mataji ya mwaka 2016 na 2017 nao Namibia walifika fainali ya mwaka 2004 na 2016.

Kabla ya Kombe la Afrika, Kenya itakuwa na mashindano ya kitaifa ya raga ya wachezaji saba kila upande kutoka Julai 20 hadi Septemba 8 yatakayojumuisha duru za Kakamega, Kabeberi, Dala, Prinsloo, Christie na Driftwood.

Mabingwa hawa wa Afrika mwaka 2004, 2008, 2013 na 2015 hutumia mashindano haya kutafuta talanta zaidi ya kuimarisha kikosi cha Shujaa kabla ya Raga ya Dunia ya msimu unaofuata.

Utaratibu

Mataifa ya Fiji, Marekani, New Zealand na Afrika Kusini, ambayo yalimaliza Raga ya Dunia ya msimu 2018-2019 katika nafasi nne za kwanza, yalifuzu kushiriki Olimpiki mwaka ujao. Yaliungana na wenyeji Japan, ambao hawatakosa Raga ya Dunia msimu ujao baada ya kutemwa Jumapili na nafasi yao kujazwa na Jamhuri ya Ireland.

Msimamo wa Raga ya Dunia msimu 2018-2019: Fiji (alama 186), Marekani (177), New Zealand (162), Afrika Kusini (148), Uingereza (114), Samoa (107), Australia (104), Ufaransa (99), Argentina (94), Scotland (72), Canada (59), Uhispania (49), Kenya (37), Wales (31), Japan (27).

Aidha, timu ya Kenya ya wanawake almaarufu Lionesses pia itawania tiketi ya Olimpiki kwenye Kombe la Afrika dhidi ya Uganda, Zimbabwe, Madagascar, Senegal, Botswana, Zambia, Morocco, Mauritius, Afrika Kusini, Ghana na wenyeji Tunisia mwezi Oktoba.

Mshindi ataungana na Japan (mwenyeji), New Zealand na Marekani (nambari moja na mbili kutoka Raga ya Dunia) na Brazil iliyochabanga Colombia 28-15 katika fainali ya Amerika Kusini Juni 2.

Timu zitakazokamilisha mashindano ya Afrika katika nafasi ya pili na tatu zitaingia mchujo wa mwisho wa dunia.

You can share this post!

Nyeri kupata kiwanda cha maparachichi

Allegri, Lampard, Vieira sasa pazuri kumrithi Sarri Chelsea

adminleo