• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Kaunti yachora upya ramani ya ardhi za umma kuepusha unyakuzi

Kaunti yachora upya ramani ya ardhi za umma kuepusha unyakuzi

Na SAMUEL BAYA

SERIKALI ya Kaunti ya Kilifi imeanza mikakati ya kupima ardhi zote za umma katika kaunti hiyo ili kujua jinsi ambavyo itazisimamia na kuzilinda kutoka kwa wanyakuzi.

Waziri wa Ardhi katika Kaunti ya Kilifi Bw Charles Karisa alisema kuwa hatua hiyo itawezesha kwa kaunti kufahamu fika zile ardhi za umma na zile zilizoko katika mikono ya kibinafsi.

“Tumeratibu maeneo 16 ya miji kufikia sasa ikiwemo Mtwapa, Mariakani, na Kaloleni. Hata hivyo kwa sasa tunasubiri wabunge warudi kutoka kwa likizo ili wajadili ripoti hiyo,” akasema Bw Karisa.

Aidha aliongeza kwamba hatua hiyo inatarajiwa kutatua shida ya umiliki wa ardhi ambao imekuwa ikizikumba sehemu nyingi za kaunti hiyo.

Tamko la waziri huyo linajiri wakati ambapo kumeshuhudiwa visa kadhaa vya uvamizi wa ardhi katika maeneo kadhaa ya kaunti hiyo ikiwemo Mtwapa na Kilifi.

“Kama kuna tatizo la watu kufurushwa katika maeneo yao, basi tatizo hilo linafaa kunifikia hata mimi katika afisi. Kwa mfano tukio lililotokea katika eneo la Mtwapa, sisi kama serikali ya kaunti hatukujulishwa kamwe,” akasema Bw Karisa.

Aidha waziri huyo alisema kuwa upimaji wa ardhi hiyo utawezesha kaunti kupanga jinsi ambavyo ardhi za kibinafsi zinazokaliwa na maskwota zitashughulikiwa.

“Mara nyengine unaangalia na kuona kweli maskwota wako katika ardhi yao. Wengine wameishi katika ardhi hiyo na ukifika pale unaona kuna makaburi na dalili zengine za kuonyesha kwamba hapo ni kwao. Hawa sio watu ambao unaweza kuamka asubuhi na kutaka kuwafukuza,” akasema Bw Karisa.

Naibu kiongozi wa walio wengi katika bunge la Kilifi Bw Sammy Ndago alisema kuwa bunge litatenga kiwango fulani cha fedha kwa kamati ya ardhi ili kuzungukia maeneo yenye matatizo na kutathmini hali halisi.

“Tumegundua kwamba hii ni shida kubwa na inayohitaji suluhu la mapema. Sasa kile ambacho tunapanga kufanya ni kuhakikisha kama bunge tunapanga fedha kwa kamati ya bunge ili tuweze kuzungukia maeneo hayo na kupata suluhisho la kudumu,” akasema Bw Ndago.

Bw Ndago pia ni mwakilishi wa wadi ya Shimo La Tewa katika eneo bunge la Kilifi Kusini.

Mwenyekiti wa kamati ya bunge la kaunti kuhusu ardhi Bw Edward Dele alisema kuwa suala hilo limekuwa tatizo kubwa na kumtaka Gavana Kingi kuingilia kati.

“Kama bunge la kaunti, tungelitaka Gavana wa Kilifi Bw Amason Kingi pamoja na naibu waziri wa ardhi Bw Gideon Mung’aro kuingilia kati na kutafuta suluhisho la kudumu kuhusiana na tatizo hili,” akasema Bw Dele.

Mbunge wa Kilifi Kusini Bw Ken Chonga alisema kuwa atawasilisha mswaada katika bunge la kitaifa ili kuzipatia nguvu serikali za kaunti kusimamia masuala ya ardhi.

“Kumekuwa na tatizo la ardhi za Kilifi kunyakuliwa na mabwenyenye huku wakazi wakifukuzwa na kuteseka. Hii inatokana na sababu ya kuwa serikali za kaunti hazijpatiwa fursa kubwa ya kushugulikia masuala haya.

Ndio maana ninataka kupeleka mswaada bungeni ili kuhakikisha kwamba shida hii inaisha,” akasema Bw Chonga.

You can share this post!

Ukabila umepitwa na wakati, tupendane – Lonyangapuo

Mganga amchemsha mtoto mchanga na kumuua akidai ni tiba

adminleo