• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
KAULI YA MATUNDURA: Nilivyomrai Prof Senkoro kuitoa upya riwaya yake ya ukombozi ya Mzalendo iliyochapishwa na Shungwaya 1977

KAULI YA MATUNDURA: Nilivyomrai Prof Senkoro kuitoa upya riwaya yake ya ukombozi ya Mzalendo iliyochapishwa na Shungwaya 1977

Na BITUGI MATUNDURA

HIVI majuzi, katika pekuapekua ya maktaba yangu, nilipata riwaya ya Mzalendo (Shungwaya Publishers, 1977) iliyoandikwa na Fikeni Senkoro wa Tanzania.

Prof Fikeni Senkoro ni mmoja wa waandishi na wahakiki wa fasihi ya Kiswahili walioacha taathira kubwa mno katika taaluma hizo mbili; uhakiki na uandishi wa kubuni.

Mzalendo ni riwaya ambayo kimsingi imesheheni maudhui ya juhudi za siasa za ukombozi kutokana na utawala dhalimu wa wabeberu.

Kwa bahati mbaya, kampuni ya Shungwaya Publishers Ltd ilisambaratika baada ya kuitoa riwaya ya mwandishi huyu.

Mara yangu ya kwanza kukutana na Prof F. E. M. K Senkoro ilikuwa ni katika kongamano la wataalamu wa Kiswahili lililofanyika mjini Arusha, Tanzania mnamo 2002.

Kipindi hicho, nilikuwa ndio ninainukia katika usomi.

Hivi majuzi, sadfa ilinikutanisha naye tena kwenye kundi la WhatsApp la wataalamu wa Kiswahili ambao ni wanachama wa Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (CHAUKIDU).

Kwa hiyo, nilisema naye chemba: “Shikamoo Prof Senkoro! Natumai hujambo. Riwaya yako hii (Mzalendo) uliichapisha mnamo 1977 na Shungwaya. Kampuni hii iliporomoka. Je, mbona usiitoe upya kazi hii na mchapishaji mwingine?”

Prof Senkoro alinishukuru kwa ushauri huo alioutaja kuwa mzuri.

Hata hivyo, alinifahamisha kwamba mimi si mtu wa kwanza kuwahi kumpa ushauri wa aina hiyo.

“Watu wengi wamekuwa wakinishauri hivyo lakini ninasita kidogo. Labda nitakaporudia kuisoma tena na tena nitaitolea uamuzi,” akasema.

“Salamu za huko Kenya?” akaniuliza.

“Kenya kwema Prof. Tumefanya maombi juzi kuukemea ufisadi. Hapa wizi tu. Unasita kwa nini Prof?” Nikasaili.

“Riwaya hiyo ni ya zamani. Nilikiandika kitabu hicho nikiwa kijana mno,” akasema Prof Senkoro.

“Mimi ninaamini kwamba huo ndio ulikuwa mchango wako kipindi hicho. Kwa hiyo, riwaya yako inaonyesha jinsi ulivyokuwa unafikiria kipindi hicho. Mimi ninapendekeza ukitoe kitabu hicho upya jinsi kilivyo. Wasomi tunajua kwamba mawazo na mitazamo ya Prof Senkoro vimebadilika. Kwa hiyo, wahakiki wataiangalia riwaya yako kwa mkabala huo – wasomaji wataisoma riwaya yako kwa jicho la Senkoro wakati huo, na Senkoro hivi sasa,” nikamrai.

Kufumbata mambo ya kipindi

Aidha nilishadidia kwamba fasihi hufumbata mambo ya kipindi pamoja na mazingira kazi hiyo inamotungwa.

Prof Senkoro alionekana kukubali ushawishi wangu wa kuitoa upya riwaya hiyo na kusema kwamba atanitwika jukumu la kuliandikia dibaji toleo jipya.

Kazi nzuri za fasihi ambazo zilichapishwa na makampuni ya uchapishaji ambazo zilisambaratika ni nyingi.

Tungo nyingi za Shaaban Robert kwa mfano zilichapishwa na kampuni ya Nelson Brothers, Uingereza.

Kwa zaidi ya mwongo mmoja vitabu vya Shaaban Robert ambaye yadaiwa kuwa ni mmoja wa watunzi maarufu kushinda wote Uswahilini – Afrika ya Mashariki na Kati havikupatikana kwa urahisi.

Kwa sababu hiyo, kuna uwezekano kwamba kuna vijana ambao hata hawamjui Shaaban Robert.

Hata hivyo, kampuni ya Mkuki na Nyota, Dar es Salaam, Tanzania ilianza kuvitoa vitabu hivyo ili kufufua tena katika mawazo ya kizazi chipukizi mchango wa mwandishi huyo muhimu.

Kwa hiyo, ni muhimu waandishi wa wachapishaji kuwazia upya hatua ya kuchapisha upya maandishi yao ambayo ama hayapatikani kwa urahisi kwa sababu ya kampuni kusambaratika au kwa sababu nyingine zile.

Kampuni ya Vide Muwa nchini Kenya imetoa mchango muhimu katika kutoa tungo za Euphrase Kezilahabi kama vile Nagona na Mzingile – ambazo zilikuwa hazipatikani Kenya.

Ninaamini kwamba Prof Senkoro atalivalia njuga pendekezo langu la kutoa upya riwaya yake – Mzalendo.

[email protected]

You can share this post!

Kilimo cha sukumawiki

VYAMA VYA KISWAHILI: Jivunio la lugha ya Kiswahili Shuleni...

adminleo