Habari Mseto

OCPD Athi River aagizwa kulinda shamba la Sh1b

June 5th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na RICHARD MUNGUTI

AFISA mkuu (OCPD) wa kituo cha polisi cha Athi River, Kaunti ya Machakos ameamriwa awafukuze wavamizi katika shamba la ekari 200 lenye thamani ya Sh1 bilioni katika barabara kuu ya Nairobi – Mombasa.

Jaji Oscar Angote alimtaka OCPD huyo aondoe matingatinga yanayoendelea kuchimba barabara katika ardhi hiyo inayozozaniwa na afisa wa zamani wizara ya ardhi Bw Philip Karonjo Ndehi na wanachama 506 cha Sunrise Vision Self Help Group ambacho mwenyekiti wake ni Joel Ndunda Kimilu.

Ardhi inapakana na kiwanda cha saruji cha Simba Cement na kilabu maarufu cha Small World.

Wakili Cecil Miller anayewakilisha Bw Ndehi alimweleza Jaji Angote kwamba wanachama wa Sunrise waliingia mle shambani na kuanza kuchimba barabara ilhali kuna agizo la mwaka wa 2015 wasiingie mle shambani.

Alisema wanachama hao wa Sunrise wamekaidi agizo la mahakama na “iwapo mahakama haitawazuia kuingia shambani basi mlalamishi hatakuwa na shamba la kustawisha.”

Pia mahakama ilifahamishwa afisu za viongozi wa Sunrise Kimilu na Charles Kyalo hazijulikani ziliko ndipo “ Miller akaomba aruhusiwe kuchapisha maagizo ya kesi hii katika gazeti ndipo wajue kesi itasikizwa Oktoba 24, 2019.”