Habari MsetoSiasa

Raila amtembelea Gavana Laboso hospitalini London

June 5th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na VITALIS KIMUTAI

KIONGOZI wa ODM, Bw Raila Odinga na Balozi wa Kenya nchini Uingereza, Manoah Esipisu Jumatano walimtembelea Gavana wa Bomet Joyce Laboso aliyelazwa hospitalini jijini London, Uingereza.

Dkt Laboso, ambaye ugonjwa unaomsumbua haujafichuliwa kwa umma, alisafiri Uingereza Mei 29, na hiyo ndiyo siku afisi yake kwa mara ya kwanza ilifichua kwamba gavana ni mgonjwa.

Picha zilizotiwa katika akuanti za Bw Odinga za Twitter na Facebook zilionyesha wakiwa kando ya kitanda cha Dkt Laboso hospitalini.

Hii ni mara ya kwanza kwa picha ya Dkt Laboso akiwa hospitalini kutolewa hadharani tangu alipolazwa wiki moja iliyopita.

Kabla ya kuelekea Uingereza, Dkt Laboso alikosa kufika afisini kwake kwa wiki tatu, hali iliyozua tetesi kwamba alikuwa mgonjwa.

Amekuwa akitafuta huduma za matibabu mara kwa mara nchini Uingereza, Amerika na India.

Kabla ya kuondoka, afisi ya gavana ilitangaza kuwa Dkt Laboso hatakuwepo kwa muda wa mwezi mmoja na anaenda kutafuta huduma za matibabu ng’ambo.

Naibu wa Gavana Hillary Barchok ndiye anayeendesha shughuli za serikali ya kaunti.

“Dkt Barchok atashirikiana na Katibu wa Kaunti, Bi Evalyne Rono na mkuu wa watumishi wa serikali ya kaunti Jayne Sigilai,” ikasema taarifa ya afisi ya gavana iliyotolewa na mkurugenzi wa mawasiliano Ezra Kirui.

Afisi ya gavana iliwaondolea hofu wakazi wa Bomet kuwa shughuli za serikali za kaunti zitakwama kutokana na kutokuwepo kwa Dkt Laboso.

“Gavana anapenda kuwahakikishia wakazi wa Bomet na washikadau wote kuwa shughuli za serikali ya kaunti zitaendelea bila kutatizika,” ikasema afisi ya gavana.