• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 5:55 AM
Wazazi wamshangaa msichana aliyekunywa sumu shuleni

Wazazi wamshangaa msichana aliyekunywa sumu shuleni

OSCAR KAKAI na ANTHONY KITIMO

MWANAFUNZI wa Shule ya Msingi ya Nasokol, Kaunti ya Pokot Magharibi amefariki huku mwenzake akilazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Moi, Eldoret baada ya kunywa sumu katika bweni lao.

Tukio hilo la Jumanne jioni limewaacha wanafunzi wenzao, wazazi na walimu na mshangao kuhusu kile kilichowasukuma wawili hao kutaka kutamatisha maisha yao.

Afisa wa upelelezi katika kaunti hiyo, Bw Michael Mwenze alisema wawili hao, Leah Cherop na Silvia Chelimo wenye umri wa miaka 14 walikunywa kemikali ya mimea.

“Tulitambua wawili hao walikunywa kemikali aina ya Neuro Trap walipojifungia ndani ya bweni na kuichanganya na maji kisha wakainywa,” alisema.

Aliongeza kuwa mlezi wa wanafunzi na mwalimu wao walipiga ripoti wakidhani wawili hao walikuwa wamehepa shuleni Jumanne kuenda michezoni mjini Makutano.

Awali, wawili hao walijitenga na wanafunzi wengine wakaonekana wakiongeleshana. Walinunua mililita 50 za sumu hiyo na kurejea shuleni jioni.

Wakati wa masomo ya jioni mwalimu wa darasa lao alikuwa akipeana sodo na kutambua hao wawili hawakuwepo ndipo wakapatikana wamelala wakiwa hali mahututi katika bweni.

“Walikimbizwa katika Hospitali ya Kaunti ya Kapenguria ambapo Leah aliaga dunia. Silvia alihamishwa hadi Hospitali ya Rufaa ya Moi, Eldoret ambapo anaendelea kutibiwa. Kemikali hiyo ilipelekwa katika mahabara ya serikali,” akasema.

Alisema kuwa wawili hao waliwachia wazazi wao maandishi kwenye kitabu wakisema, “Bye our good friend Sarah” (kwaheri rafiki yetu Sarah).

“Ushauri nasaha unafaa kupeanwa katika shule. Wazazi wanafaa kuwa karibu na wanao na kutambua kile kinawasumbua,” alisema.

Kwingineko, watoto watatu walioripotiwa kupotea Kaunti ya Taita-Taveta siku mbili zilizopita wamepatikana wakiwa wamejificha chini ya bomba la maji taka eneo la Kibarani, mjini Mombasa.

Watoto hao wawili wa miaka 12 na 11 walipatikana na polisi waliokuwa wakipiga doria saa saba usiku wa kuamkia jana.

Afisa aliyewaokoa alisema watoto hao walikuwa wamevaa sare za shule huku mdogo wao alikuwa akilia kutokana na yaliyowapata.

“Walikuwa na uoga wakati tuliwaona na baada ya kuwapa chakula na nguo za kujifunika walitueleza kwamba walikuwa wametoka Voi baada ya kutoroka kuadhibiwa na shangazi yao na walikuwa hawana pahali pa kwenda,” akasema afisa huyo aliyeomba kubanwa jina kwa vile hana idhini kuhojiwa na wanahabari.

Alisema kuna taarifa kadhaa za kukanganya kuhusiana na jinsi watoto hao waliovyotoroka nyumbani kwao kwani walikuwa wanabadilisha taarifa zao kila mara.

“Tumewakabidhi kwa idara ya jinsia katika kituo cha polisi na pia idara ya watoto imehusishwa kwa hivyo tuna hakika wataunganishwa na wazazi wao,” akasema.

Taarifa ya polisi ilionyesha kuwa watoto hao wa Shule ya Kalela iliyo Voi walitoroka na kusafiri hadi mjini Mombasa baada ya kuabiri lori eneo la Kaloleni mnamo Jumatatu asubuhi.

“Watoto hao hawakuhudhuria shule Jumatatu ndipo wazazi wao walipopiga ripoti kupotea kwao. Taarifa za watoto kutoroka inatofautiana na ile ya wali kwamba walifukuzwa na shangazi yao na ikabainika walitoroka kuepuka kuadhibiwa baada ya kuharibu baiskeli ya jirani yao. Taarifa hizo lazima zichunguzwe kwa kina” ilisoma sehemu ya taarifa hiyo ya polisi.

You can share this post!

Jubilee ni kisiki katika utekelezaji katiba – Maraga

Joho na Balala waunga mkono marekebisho ya katiba

adminleo