Marashi ya wanawake yatajwa kiini cha maradhi ya watoto
Na DIANA MUTHEU
WATAALAMU wa afya wamewaonya akina mama dhidi ya kutumia mafuta na marashi yenye harufu kali kwani yanachangia maradhi ya kupumua miongoni mwa watoto wachanga.
Dkt Wanjiru Abuto, ambaye ni daktari wa watoto katika Hospitali ya Watoto na Wanawake ya Nyali katika Kaunti ya Mombasa, alisema idadi ya watoto wenye matatizo ya kupumua wanaopelekwa hospitalini kila siku ni kubwa mno.
Katika eneo la Pwani, wanawake wengi wana desturi ya kutumia manukato kwa wingi.
“Wakati mama anapotumia manukato sana, mtoto wake huwa katika hatari ya kupata magonjwa ya kupumua. Kwa mtoto aliyezaliwa na wazazi ambao wana pumu au maradhi mengine ya kupumua, harufu kali ya marashi inaweza kuchochea shambulio la ugonjwa huo kwa watoto wadogo,” akasema Dkt Abuto.
Kulingana naye, marashi haya husababisha pua za mtoto kuziba, kukohoa na kushindwa kupumua.
Daktari huyo aliwashauri wanawake wenye watoto wadogo kuepuka marashi haya na kudumisha tu usafi wa mwili lakini kama ni lazima watumie manukato, basi watumie yasiyokuwa na harufu kali.
“Epukeni mafuta, marashi na bidhaa nyingine kama taulo nyevunyevu za kufuta watoto zenye harufu kali wakati mnaposhughulikia watoto. Tunaweza kunukia vizuri kwa kuosha miili kwa sabuni na maji tu na kubadili nguo zetu kila siku, hasa katika hali ya hewa kama ya Mombasa ambako kuna joto jingi,” Dkt Abuto aliongeza.
Kwa watu wenye matatizo ya kutoa harufu mbaya mwilini, Dkt Abuto alisema wanaweza kutafuta matibabu kwa kuwa wanaweza kuwa na bakteria nyingi katika sehemu husika.
Kulingana na makala moja iliyochapishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa jina Children and Chemicals, kemikali nyingi zinadhuru watoto. Kemikali hizi hupatikana katika bidhaa za nyumbani, vifaa vya ujenzi, vumbi, vipodozi visivyofaa kama vile manukato, sabuni na bidhaa nyingine za usafi.
Maoni sawa na haya yalitolewa na Dkt Mwanaisha Hatimy, ambaye ni daktari wa watoto katika Hospitali ya Aga Khan, Mombasa.
Alisema kuwa madhara yanayosababishwa na marashi yanaweza yakaathiri maisha ya watoto hasa ukuaji wao na pia masomo yao.
Dkt Hatimy aliongeza kuwa watoto wengi walio chini ya miaka mitano wana hatari kubwa ya madhara yanayosababishwa na manukato.