• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 1:05 PM
Wakuu wa shule waanza kikao wakilia madeni

Wakuu wa shule waanza kikao wakilia madeni

Na WAANDISHI WETU

Walimu wakuu zaidi ya 9,000 wa shule za sekondari wataanza mkutano wao wa kila mwaka mjini Mombasa huku shule za umma zikikabiliwa na changamoto tele za kifedha.

Walimu hao watakusanyika katika ukumbi wa Taasisi ya Ushuru nchini (KESRA) iliyoko eneo la Nyali katika barabara kuu ya Mombasa-Malindi.

Wanalia kwamba shule za upili nchini zinakabiliwa na milima ya madeni zinazodaiwa na wafanyabiashara kutokana na kupungua kwa ufadhili kutoka serikali kuu.

Madeni mengi yanatokana na gharama ya chakula.

Kuanzia wiki jana, Rais Uhuru Kenyatta alipoamuru asasi zote za serikali zilipe malimbikizi ya madeni kufikia Juni 30, walimu wakuu wa shule 9,000 za upili kote nchini wamekuwa wakiwekewa presha na wafanyabiashara waliowauzia bidhaa na kutoa huduma.

Changamoto hiyo imeongezwa na amri ya serikali kwamba wanafunzi wote wasajiliwe upya chini ya mfumo wa kidijitali (NEMIS). Hali hii imefanya wanafunzi wasiokuwa na vyeti vya kuzaliwa kukosa pesa kwa sababu maelezo yao hayakunakiliwa katika mfumo huo.

Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Wakuu wa Shule za Upili (Kessha), Kahi Indimuli, alisema chama hicho hakiwezi kukadiria kiasi cha pesa ambazo shule zinadaiwa na wafanyabiashara waliowasilisha bidhaa na huduma.

“Kila shule inadaiwa kivyake,” akasema Bw Indimuli ambaye aliungama kuwa taasisi hizo zinakabiliwa na changamoto za kifedha.

Baadhi ya shule zimeamua kuandaa harambee ili kupata pesa za kufadhili ujenzi wa madarasa, mabweni na vyoo zaidi licha ya wizara ya elimu kutenga Sh1.5 bilioni za kufadhili ujenzi wa miundo msingi. Hata hivyo, wizara imeungama kuwa fedha hizo ni kidogo na ndipo ikaamuru shule za upili za mabweni kutumia Sh6,000 kati ya Sh22,000 ambazo huwa zinapokea kwa kila mwanafunzi, kufadhili ujenzi wa miundo msingi.

Hata hivyo, Bw Indimuli amesema shule za upili zinahitaji kutengewa Sh9 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa miundo msingi zaidi kufuatia ongezeko la idadi ya wanafunzi.

Shule hizo zimeshuhudia ongezeko kubwa la idadi ya wanafunzi tangu 2018 serikali ilipoanza kutekeleza mpango wa kuhakikisha kila mwanafunzi anayefanya mtihani wa kitaifa wa darasa la nane (KCPE) anasajiliwa katika kidato cha kwanza.

Uchunguzi

Mwaka 2018, Tume ya Kuajiri Walimu Nchini (TSC) iliamuru uchunguzi kufanywa kuhusu madai ya wizi wa pesa katika shule mbalimbali hali iliyosababisha kuhamishwa kwa baadhi ya walimu wakuu wa shule ambako maswali kuhusu matumizi mabaya ya fedha yaliibuliwa.

Hii ni baada ya walimu wakuu wapya kugundua kwamba wenzao waliohamishwa walipora pesa za shule na kuacha akaunti zikiwa tupu huku zikiwa na mzigo mzito wa madeni.

Shule za wanafunzi wenye mahitaji maalum pia zinakabiliwa na changamoto za kifedha. Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Wakuu wa shule hizi Arthur Injenga anasema kuwa zaidi ya shule 200 zimeshindwa kulipa madeni yao kutokana na matatizo ya kifedha.

“Tumekuwa tukiomba fedha kutoka kwa serikali kuu tangu Februari mwaka huu. Nyakati zingine tunashangaa ni jinsi ipi serikali inatarajia tuwatunza wanafunzi bila kutupa rasilimali za kutosha,” akaongeza Bw Injenga huku akisema nyingi za shule hazijapata mgao wa fedha kutoka kwa serikali.

You can share this post!

Ruto kusaidia familia ya mtoto aliyegongwa na msafara wake

Shughuli ya kuwapiga msasa polisi wa akiba itaimarisha...

adminleo