• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 3:25 PM
Askofu amuonya Uhuru dhidi ya kumsaliti Ruto 2022

Askofu amuonya Uhuru dhidi ya kumsaliti Ruto 2022

Na MWANGI MUIRURI

MWENYEKITI wa Muungano wa Dini Asili eneo la Mlima Kenya, Askofu Lukas Ndung’u Jumapili amemuonya rais Uhuru Kenyatta dhidi ya ‘kumsaliti’ naibu wake, William Ruto katika siasa za urithi za 2022.

Amesema kuwa “ikiwa utatuelekeza kumsaliti Ruto 2022, tunakupenda na ndio sababu tulikuchagua kuwa rais, lakini kwa hilo la Ruto utatusamehe kama Wakristo. Tutakukaidi.”

Alisema kuwa ikiwa rais Kenyatta ataelekeza Mlima Kenya kupiga kura nje ya debe la Ruto 2022, basi watakaidi kwa kuwa wanajihisi kama walio na wema wa kulipa kwa Ruto kwa kuwaunga mkono kwa dhati katika chaguzi za 2013 na 2017.

“Sisi kama Wakristo tunajua kuwa wema hulipwa kwa wema. Tunajua kwamba Ruto angeungana na wapinzani wa Uhuru Kenyatta 2013 na 2017 leo hii hatungekuwa tunajivunia kuwa na rais wa jamii yetu,” akasema akihubiri katika kanisa la Calvary Evangelism Centre, mtaani kabati Kaunti yaMurang’a.

“Alisema kuwa “wakati rais Uhuru Kenyatta alisimama mbele ya dunia nzima baada ya uchaguzi wa 2013 na kumwahidi Ruto urithi huo wa ikulu, basi ni jamii nzima ambayo aliingiza katika mkataba wa deni la 2022.”

Alisema kuwa kwa sasa hakuna lingine ila tu kufuata Ruto hadi kwa debe la urais 2022 “ikizingatiwa kuwa jamii zote zinatutazama zione kama sisi ni watu wa kutoa ahadi na kuheshimika katika kufuata deni hilo la deni.”

Alisema kuwa usaliti ni moja ya maovu ambayo Mungu hapendi kamwe na kumsaliti Ruto kwa msingi wowote hata ukiwa ni wa kisiasa ni sawa na kutuhumu jamii nzima kuwa ya wakatili wa ahadi na usaliti.

Alisema kuwa ako na maono kuwa Ruto ndiye atakuwa rais wa tano nchini Kenya na atastahimili mipigo ya mahasidi wa kisiasa kuibuka kidedea baada ya kura kujumlishwa.

Askofu Nd’ungu amesema kuwa wale wote wanaompinga Ruto wanafaa waelewe kuwa ni haki yao ndiyo kufanya hivyo, “lakini unaposaka bahati yako ya kuibuka na manufaa yako ya kibinafsi kuhusu urithi huo, tuzingatie ustaarabu, ukweli na haki ya usawa katika ushindani.”

Askofu Ndung’u alisema kuwa kunao ambao humwangazia Ruto kama asiye na maadili ya kiuongozi hasa kuhusishwa na ufisadi.

“Lakini huwa unatwambia sisi watu wa kawaida ndio tumfanyie nini? Unajua vizuri kuwa vitengo vya kupambana na ufisadi viko na wafanyakazi ambao hulipwa mishahara wawajibike hilo.

“Mbona usiende kuwapa ushahidi lakini unakuja kwetu ambao kwa unyonge wetu hatuna lingine la kufanya ila tu kukusikiliza ukitwambia? akahoji.

You can share this post!

Alianza kwa kuuza chupi lakini sasa ni mmiliki wa kampuni

2022: Kivumbi Mlima Kenya kura zake...

adminleo