• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 12:04 PM
2022: Kivumbi Mlima Kenya kura zake zing’ang’aniwa kama mpira wa kona!

2022: Kivumbi Mlima Kenya kura zake zing’ang’aniwa kama mpira wa kona!

Na MWANGI MUIRURI

ENEO la Mlima Kenya kwa sasa limo katika mkondo telezi wa kisiasa kuhusu urithi wa urais 2022; huku kura zake zikibishaniwa kwa hila na njama na washindani.

Ni eneo ambalo wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa linabishaniwa na mirengo mitatu mikuu ya kisiasa—ule wa Rais Uhuru Kenyatta, Naibu wake William Ruto na mrengo wa Kinara wa Upinzani, Raila Odinga.

Ni eneo ambalo takwimu za Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) linaorodhesha kuwa na utajiri mkuu wa kura na ambazo kila anayelenga urais 2022 anapangia njama ya kuzitwaa, hivyo basi thamani ya kura hizi itang’ang’aniwa kama mpira wa kona.

Katika takwimu hizo za IEBC za 2017, Kaunti ya Kiambu ilikuwa na wapiga kura 1,173,593, za Meru zikiwa 712,378, Murang’a kukiwa na 590,775 huku Nyeri ikisajili wapiga kura 460,806.

Kaunti ya Kirinyaga ilikuwa na 351,162 huku ile ya Nyandaua ikiwa na 336,322, huku Embu ikiwa na 315,668, Laikipia 239,497 nayo Kaunti ya Tharaka Nithi ikiwa na kura 216,522.

Kwa mujibu wa mchanganuzi wa masuala ya kisiasa, Prof Macharia Munene, umuhimu mkuu wa kura hizi za Mlima Kenya ni kwamba hushawishi pia vile wenzao katika Kaunti zingine kama za Rift Valley, Pwani na Nairobi watapiga kura.

Na katika malumbano ya mirengo hiyo yote ikisaka kutwaa ushawishi wa kura hizi, na ambayo ndiyo kiini kikuu cha misukosuko ya kisiasa ambayo imekumba eneo hilo, wenyeji wanaonywa kuwa matokeo huenda yakawa wajikwae kisiasa na waishie kuwa katika upinzani 2022 wakiwa wametengwa na jamii zingine.

“Ni wakati ambao eneo hili linahitaji umoja wa kiusemi. Kunahitajika umoja wa kisiasa na tufanye maamuzi yetu kwa msingi wa kushirikiana na wengine, kufuata kule masilahi yetu yatapata afueni na la maana kuu, kule ambako wingi wa kura zetu utaheshimiwa ,” asema aliyekuwa gavana wa Kiambu, William Kabogo.

Anasema kuwa hadi sasa, majina ya kutazamia kuwa katika ushindani wa urais ni yale ya Ruto, Raila, Musalia Mudavadi, Kalonzo Musyoka, Gideon Moi na Ali Hassan Joho “bila kusahau kuwa hakuna sheria inayomkanya yeyote wa Mlima Kenya kuwania.”

Kabogo akijiunga na Moses Kuria kutangaza uwaniaji wa urais anasema kuwa sasa ni wakati wa kujipanga kwa wenyeji wa Mlima Kenya kwa ueledi mkuu wasije wakajipata wamechuuzwa katika siasa za majuto ya baadaye.

Kwa mujibu wa Mbunge wa Bahati, Kimani Ngunjiri, mrengo wa rais unalenga kutumia eneo hilo kumpa uthabiti wa baada ya uongozi wake Ikulu kupitia kumtegemea kutoa mwelekeo wa 2022.

Anasema kuwa nao mrengo wa Ruto unalenga hakikisho la mapema kuwa kura hizi zote zitamwendea kwa kapu lake akiwania urais wa 2022, huku naye Raila akilenga kuzigawa kura hizo aidha zimfae au zikisambaratika, hesabu yake ya kisiasa iingiane kwa kunyima Mlima Kenya ubabe wa umoja wa kura katika ujumlishaji wa kutafuta mshindi wa urais.

Ni hali ambayo imezua mijadala mikali mashinani, bayana wengi wakiwa wamechanganyikiwa, lakini mwishowe kukitokea mirengo miwili ambayo mmoja unatazamia familia ya Kenyatta kuendelea kuthibiti maamuzi yao kiasiasa lakini mwingine ukisaka uhuru wa kujiamulia hatima ya kisiasa.

Walio katika mrengo wa kusaka uhuru wao wa kisiasa nao wamegawanyika katika mirengo kadhaa, mmoja ukimuunga mkono Dkt Ruto huku wengine wakijigawa katika mirengo ya Raila na wengineo, lakini kukiwa na idadi ya wengine ambao wanasema kuwa wamechoka na kupiga kura kila mwaka wa uchaguzi lakini kuishia kuhangaika katika utawala usio na maendeleo.

Kelele hizi za wengi kuhisi kwamba utawala wa Rais Kenyatta haukuwafaa kimaendeleo katika awamu ya kwanza, taharuki ikitanda kuwa katika awamu hii ya pili mwaka mmoja nao umeisha bila kuona maendeleo halisi, Kuria akatetesha rais.

Ingawa baadaye aliomba msamaha, hali imebakia kuwa katika eneo hilo Kuria amejipa umaarufu kwa kusema yale ambayo yako katika nyoyo za wengi lakini wakiwa na uoga wa kuyasema hadharani.

Kabogo anasema kuwa hakuna geni ambalo Kuria amesema kwa kuwa “nilisema haya mwaka wa 2016 nikiwa katika Kaunti ya Kirinyaga nilipomwambia rais Kenyatta asiogope kutupa maendeleo kulingana na wingi wa kura zetu.”

Anasema kuwa hata waliokuwa wakimpigia debe Rais Kenyatta Mlima Kenya wakisaka awamu yake ya pili Ikulu walikuwa na ushahidi kuwa hakuna haki ya kimaendeleo ilikuwa imetekelezewa watu wa Mlima Kenya.

“Walikuwa wanakiri kuwa eneo hilo lilikuwa limetengwa lakini wakituahidi kuwa awamu ya pili ya rais Ikulu ingekuwa ya kututuza kwa kusimama naye kufa kupona katika debe la kura. Waliahidi lakini sasa wanaruka…” asema Kabogo.

Suala hilo la maendeleo ndilo linamtatiza rais Kenyatta kiasi cha kujihisi amesukumwa pembeni na kuishia kuwasuta makuhani wa mjadala huo kama “Washenzi.”

Prof Munene anasema kuwa wanaomsukuma rais hadharani wanajikosea kwa kuwa “rais sasa akishawishika na afululize mikoba ya ufadhili wa maendeleo hadi Mlima Kenya, atasutwa na maeneo mengine kama mbaguzi na mkabila.”

Katika hali hiyo, rais akijipata katika njia panda, atakosa kuafikia malengo yake manne ya hadi 2022 na hivyo basi akose ule ushawishi anaohitaji kupanga mwelekeo wa kisiasa wa wenyeji wa Mlima Kenya 2022.

Kwa upande mwingine, Ruto akijumuisha wengi wa viongozi Mlima Kenya katika mrengo wake anaendelea kujipigia debe eneo hilo huku akizua mjadala wa ikiwa wapiga kura wa eneo hilo wako na deni lake la kisiasa.

Kwa mujibu wa Seneta wa Murang’a, Irungu Kang’ata “tuko na deni kwa kuwa isipokuwa ni Ruto, rais Kenyatta hangeshinda uchaguzi wa 2013 na ule wa 2017.

Ni vyema tuwe wastaarabu wa kuweka ahadi kwa kuwa kila Mkenya aliye na uwezo wa kufuatilia matukio ya kisiasa amewahi kumsikia Rais akimuahidi Ruto urithi.”

Anasema kuwa “itakuwa ni aibu, uhaini na usaliti mkuu kumnyima Ruto kura ikiwa siku ya uchaguzi jina lake litakuwa miongoni mwa wawaniaji.”

Lakini kunao walio na uhusiano na Mlima Kenya, kama aliyekuwa mbunge wa Molo, Joseph Kiuna wanaosema kuwa mrengo wa Ruto unatumia vitisho vya ghasia 2022 iwapo hataungwa mkono na wapiga kura hao.

“Hapa ndipo tena kunazuka mrengo mwingine wa ukaidi Mlima Kenya ambao unakataa kushinikizwa utoe ufuasi wao kwa Ruto kwa msingi wa kuhakikishiwa amani Rift Valley. Hatuwezi tukapangwa kisiasa kupitia kutandaziwa uoga,” asema Kiuna.

Naye aliyekuwa Mbunge wa Maragua, Elias Mbau ambaye huwa katika mrengo wa Raila Odinga anasema kuwa “siasa za Mlima Kenya zitakaidi neno la Rais Kenyatta ikiwa atawaelekeza wenyeji kuunga mkono Ruto.”

Anasema kuwa kwa sasa siasa za Mlima Kenya ziko huru kwa kuwa ni za mpito na ambapo kuna zile hisia kwamba hata mwingine kutoka nje ya jamii hiyo anaweza akachaguliwa na aongoze taifa hili.

Anasema kuwa mrengo wa kuaminika ni ule unaohusisha “msemaji wa Gema ambaye bado hatujamteua, Seneta wa Baringo Gideon Moi na Raila.”

You can share this post!

Askofu amuonya Uhuru dhidi ya kumsaliti Ruto 2022

Walimu waunga mkono wabunge SRC ivunjwe

adminleo