• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 1:14 PM
Madiwani wanavyoteseka baada ya kubwagwa uchaguzini 2017

Madiwani wanavyoteseka baada ya kubwagwa uchaguzini 2017

NYAMBEGA GISESA na LUCY MKANYIKA

MADIWANI walioshindwa kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2017 wanakumbwa na shida tele baada ya kuishi maisha ya kifahari katika muhula wa kwanza wa serikali za ugatuzi.

Wengi waliozungumza na Taifa Leo walisimulia maisha yenye shida tele tangu walipopoteza viti vyao.

Aliyekuwa Diwani wa Mwanda/Mghange katika Kaunti ya Taita Taveta, Bw Cromwell Baridi anaandamwa na madeni yaliyomlemea kulipa.

Anasema alipokuwa diwani alikuwa akipokea mshahara mnono na marupurupu, kuendesha magari ya kifahari likiwemo rasmi la bunge la kaunti na kulala katika hoteli za kifahari.

Mwezi uliopita, karani wa bunge la kaunti hiyo, Bw Gadiel Maghanga alianzisha shughuli ya kumtaka diwani huyo wa zamani alipe madeni yake ya jumla Sh2.5 milioni ya mkopo wa gari na nyumba.

“Sijui nitalipa madeni hayo lini kwa sababu sina pesa kwa sasa. Sijakataa kulipa pesa hizo lakini bunge la kaunti linafaa kushauriana nasi badala ya kutupa vitisho. Nina madeni hata kwingine pia,” akasema Bw Baridi.

Anasema alitumia zaidi ya Sh10 milioni katika kampeni za uchaguzi wa 2017 wakati alipowania ubunge Wundanyi lakini akashindwa.

Masaibu yake ni sawa na ya madiwani wengine wengi walioangushwa 2017.

Katibu Mkuu wa Chama cha Madiwani Waliotangulia, Bw James Kagoni, alisema kuna madiwani kati ya 2,000 na 2,400 ambao walishindwa mwaka uliopita, na wengi wao wanateseka kimaisha.

“Kuna wengine wamerudi kuishi na wazazi wao na baadhi wanatatizika kiakili hadi wengine wao wamejitoa uhai,” akasema.

Aliyekuwa diwani katika Kaunti ya Kiambu, Bw Arthur Munga, alisema amelazimika kuhamia Mai Mahiu ambako sasa ni mhudumu wa bodaboda.

Katika Kaunti ya Kisii, aliyekuwa Diwani wa Riana, Obote Motoni alianza kuendesha teksi, naye Zipporah Osoro katika Kaunti ya Nyamira akifanya biashara ya kuuza nguo za wanawake.

Katika Kaunti ya Murang’a, aliyekuwa Diwani wa Kamahuha, Bw John Njoroge anafanya kazi katika kampuni ya utoaji bima, naye aliyekuwa Diwani wa Kariara, Muhoro Njeri akianzisha biashara anayosema inajikokota.

“Ninajaribu kuuza bidhaa za mafuta lakini sipati faida. Huwa ninatoa pia huduma za uchukuzi kwa lori langu,” akasema Bw Njeri.

Alisema kutokana na jinsi walivyokuwa wakikagua vikali utawala wa magavana na hata wengine kutishia kuwaondoa mamlakani, imekuwa vigumu kwao kupata kandarasi katika kaunti zao kwani bado wanaonekana kama maadui wa magavana.

You can share this post!

Dawa na teknolojia huchangia maradhi ya zinaa –...

2022: Masaibu ya Ruto yaongezeka Kalonzo akiungana na Moi

adminleo