Gavana anyakwa kwa kung'oa majani chai
TOM MATOKE na RUSHDIE OUDIA
GAVANA wa Nandi Stephen Sang’, Jumatatu alibebwa hobelahobela na kusukumwa kwenye gari la polisi kutokana na kisa cha Jumamosi cha kung’oa majani chai ya kampuni ya Kibwari.
Makachero kutoka Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) walimkamata gavana huyo ambaye anadai kwamba kampuni hiyo ipo katika ardhi iliyonyakuliwa.
Makachero hao kisha walimpeleka hadi mjini Kisumu ambako alihojiwa kuhusu kisa cha Jumamosi.
Mwanasiasa huyo aliwasili mjini Kisumu chini ya ulinzi mkali na kufikishwa katika kituo cha polisi cha Central alikoandikisha taarifa huku baadhi ya wafuasi wake wakifuata gari la polisi hadi jiji la Kisumu.
Awali, polisi walilazimika kutumia vitoa machozi kutawanya umati ulioandamana na gavana huyo alipoenda kurekodi taarifa katika kituo cha polisi cha Kapsabet.
Mkuu wa polisi eneo la Nyanza, Dkt Vincent Makokha alithibitisha kwamba walikuwa wakimzuilia Bw Sang’ kutokana na makosa aliyoyatenda siku za Ijumaa na Jumamosi.
Dkt Makokha alipuuzilia mbali habari za amri ya korti iliyowazuia polisi kumzuilia Bw Sang’, na akaahidi kuwaeleza wanahabari leo iwapo kiongozi huyo atafikishwa katika mahakama ya Kisumu, Kakamega au Nandi.
Mnamo Jumapili, mkurugenzi wa mawasiliano katika ofisi ya gavana huyo, Gideon Cise, alikanusha kwamba polisi walikuwa wakimsaka bosi wake kwa kuwaongoza wenyeji kung’oa majani chai ya kampuni ya Kibwari.
Bw Cise alisema Bw Sang’ alikuwa huru na alikuwa tayari kushirikiana na maafisa wa uchunguzi kuhusu suala hilo.