Habari Mseto

Raia wa Pakistan kizimbani baada ya kunaswa na mali ya Sh75m

June 10th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na RICHARD MUNGUTI

RAIA wawili wa Pakistan walishtakiwa Jumatatu kwa kupatikana na bidhaa zenye thamani ya Sh75 milioni zilizoingizwa nchini kinyume cha sheria..

Sheraz Ali na Muzamil Abbas walikanusha mashtaka matatu dhidi yao.

Wakiomba waachiliwe kwa dhamana , wawili hao walimweleza hakimu mkuu Francis Andayi kuwa bidhaa walizopatikana nazo zilikuwa za mwajiri wao ambaye hayuko nchini kwa sasa.

Waliomba waachiliwe kwa dhamana . Upande wa mashtaka ukiongozwa na Bi Kajuju Kirimi ulipinga wakiachiliwa kwa dhamana akisema “watachana mbuga kwa vile wanafanya kazi nchini bila vibali.”

Bi Kirimi aliomba washukiwa hao wazuiliwe kwa muda wa siku tano Parklands kuhojiwa na kumtambua mwenye bidhaa hizo.

Bw Andayi aliwaachiliwa kwa dhamana ya Sh1 milioni na kuwaamuru wamtafute raia wa Kenya awasilishe kitambulisho chake mahakama kama “dhamana kuwa wageni hao hawatatoroka mbali watafika mahakamani siku ya kusikizwa kwa kesi.”

Kesi hiyo itatajwa Ijumaa.