Habari Mseto

Kesi ya ada ya nyumba yafikishwa kwa Maraga

June 10th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA ya kuamua mizozo baina ya waajiri na wafanyakazi (ELRC) Jumatatu iliamuru kesi ya ada ya nyumba ipelekwe kwa Jaji Mkuu David Maraga kuteua jopo la majaji watatu kuisikiza.

Jaji Maureen Onyango aliamuru kesi iliyowasilishwa na Muungano wa Kuwatetea Wafanyakazi (Cotu), shirikisho la waajiri nchini (FKE) na mwanaharakati Okiya Omtata ipelekwe kwa Jaji Maraga kuteua jopo la majaji watatu kuamua kesi hiyo.

Jaji Onyango alisema kesi inazua masuala mazito ya haki za wafanyakazi na kwamba lazima iamuliwe na majaji zaidi ya mmoja.

“Kesi hii inazua masuala mazito ya kisheria na kikatiba. Inapasa kusikizwa na kuamuliwa na jaji zaidi ya mmoja kwa vile iko na umuhimu mkuu kwa umma,” alisema Jaji Onyango.

Jaji huyo aliwaamuru mawakili wanaoshiriki katika kesi hiyo wafike mbele ya Jaji Mkuu (CJ) Ijumaa.

Pia aliamuru naibu wa msajili wa mahakama kuu awasilishe faili hiyo kwa CJ kabla ya Ijumaa.

Mahakama ilisitisha hatua ya Serikali ya kuanza kukata asili mia 1.5 ya mishahara ya wafanyakazi wote kugharamia ujenzi wa nyumba za gharama ya chini.