Makala

WAKILISHA: Mchezo wa sarakasi wampaisha mtaani

June 11th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na PAULINE ONGAJI

KATIKA eneo la Muthama, Waithaka mtaani Kawangware, jijini Nairobi, nyota amezaliwa.

Naam, nyota wa sarakasi, Stacy Juma al-maarufu Yoga, msichana ambaye licha ya umri wake mdogo, ustadi wake kama mwanasarakasi huenda ukawatia magwiji wa mchezo huu ulimwenguni tumbo joto.

Yoga ana miaka minane pekee, lakini pindi anapoingia jukwaani na kuanza kupinda viungo vya mwili wake, ni rahisi kudhani kwamba ana uzoefu wa miaka mingi.

Mwanafunzi huyu wa darasa la tatu katika shule ya msingi ya Waithaka Riverside School, eneo la Dagoretti, amekuwa kivutio cha wengi sio tu mtaani, bali pia shuleni.

Ni suala ambalo limemfanya kuruhusiwa kupiga msasa katika eneo la CDF Dagoretti na katika ukumbi wa jumba la kibiashara la Lavington Mall bila malipo.

Sasa ni takriban miezi sita tangu aanze mafunzo ya masuala ya sarakasi, fursa aliyopokea kutokana na kipaji chake cha hali ya juu.

Kwa hivyo kila Jumamosi, utampata mtoto huyu katika ukumbi wa mazoezi wa Lavington Mall.

Aidha, kila Jumatatu, Jumanne, Alhamisi na Ijumaa utampata akifanya mazoezi katika ukumbi wa CDF.

Stacy Juma. Picha/ Lucy Wanjiru

Na katika harakati hizo amekuwa fahari kwa wazazi wake, Meshack Juma na Lucy Wangare, wanaoendesha biashara mtaani Kawangware, huku akiwa kigezo cha nduguze na wanafunzi wenzake.

“Kila ninapoenda mazoezini, mimi hushuhudia watoto wenzangu na hata watu wazima wakiacha shughuli zao na kunitazama, suala linalonitia moyo zaidi,” asema Yoga.

Kulingana na babake, kipaji chake kilijitokeza akiwa angali mtoto mdogo.

“Alikuwa na miaka mitatu pekee nilipogundua jambo la kushangaza kumhusu. Wakati huo nilikuwa nafanya kazi katika hoteli moja na kila nilipowasili nyumbani alikuwa akinionyesha jinsi anavyoweza kuunda maumbo ya pembe tofauti akitumia mwili wake,” aeleza.

Mara nyingi anasema kwamba mwanawe angewatumbuiza wageni kila walipoalikwa kuhudhuria sherehe.

“Na katika harakati hizi watu wengi walivutiwa na kipaji cha binti yangu na kunihimiza nimtafutie mkufunzi,” aeleza.

Lakini kulingana na Bw Juma, hakujua angepata wapi huduma hizi wala ni vipi angeweza kumudu gharama hiyo.

Hata hivyo baada ya kufanya utafiti aligundua kituo cha ukufunzi eneo la CDF.

“Nilizungumza na mkufunzi fulani ambaye baada ya kushuhudia kipaji cha binti yangu, alifurahishwa na kumtambulisha katika kituo kingine cha mafunzo katika ukumbi wa Lavington Mall,” asema.

Kutokana na kipaji cha kipekee, Yoga anapata fursa ya kufanya mazoezi hapa bila malipo.

“Kila Jumamosi binti yangu huwa na vikao viwili vya mazoezi ambapo kila moja ni Sh1,500, pesa ambazo singemudu kulipa,” aeleza.

Kwa hivyo kila anapotoka shuleni mwendo wa saa tisa unusu, hurejea nyumbani kuoga na kupata kinywaji, kabla ya kufunga safari hadi ukumbi wa CDF kufanya mazoezi, shughuli inayoendelea kati ya saa kumi na moja na saa kumi na mbili unusu jioni.

“Kisha narejea nyumbani na baada ya mapumziko, nafanya kazi zangu za ziada za shuleni kabla ya kwenda kulala,” asema Yoga.

Ratiba hii kali imemwezesha kusawazisha masomo na mchezo huu vyema kiasi kuwa kazi yake darasani kamwe haijaathirika.

“Matokeo yake shuleni ni mazuri sana. Kwa mfano, muhula uliopita, alijizolea alama 21 kati ya 24,” aongeza Bw Juma.

Changamoto

Hata hivyo, haimaanishi kwamba harakati zake hazijakumbwa na changamoto.

“Tatizo kuu bila shaka ni pesa. Japo tumebahatika kutolipia mafunzo yake, nauli ya kwenda katika sehemu ya mazoezi na kurejea nyumbani, ni sisi tunaishughulikia,” asema.

Hii, anasema imekuwa changamoto kwao hasa ikizingatiwa kwamba pia wanahitaji kuwashughulikia watoto wengine wawili wao.

Aidha, kuna tatizo la kupata walimu.

“Kwa mfano, mmojawapo wa wakufunzi aliyekuwa akimsaidia alisafiri nchini China huku mwingine akielekea Uhispania, suala ambalo limetatiza unoaji kipaji chake,” asema Bw Juma.

Lakini shida hizi hazijamzuia kufuata ndoto yake ya kutawala nyanja hii sio tu humu nchini tu, wala barani Afrika, bali kimataifa.

“Ningependa jina langu liorodheshwe miongoni mwa magwiji wa sarakasi ulimwenguni. Pia, natamani sana wakati mmoja kuwafunza watoto wengine kuhusu mchezo huu,” asema Yoga.