• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 7:45 AM
Wavuvi waonywa kuhusu mawimbi na upepo mkali baharini

Wavuvi waonywa kuhusu mawimbi na upepo mkali baharini

Na COLLINS OMULO

IDARA ya Utabiri wa Hali ya Hewa imetoa tahadhari ya upepo mkali na mawimbi katika Bahari Hindi.

Idara ilionya Jumanne kuwa huenda upepo huo ukawa tishio kwa wavuvi ambao wataendesha shughuli katika bahari, kwani unaweza kuzamisha mashua na boti ndogo.

“Wale wanaoendesha shughuli za uvuvi baharini wanapaswa kutahadhari, kwani huenda wakakumbwa na mawimbi makubwa yanayoweza kuzamisha mashua ndogo ambazo hutumiwa na wavuvi wengi,” akasema Bw Samuel Mwangi, ambaye ni Naibu Mkurugenzi wa Idara ya Utabiri wa Hewa.

Kulingana na utabiri wa hali ya hewa wa kati ya Juni 11 na 17, hali ya mawingu itashuhudiwa katika sehemu za Kati ikiwemo Nairobi, huku mvua kubwa ikitarajiwa kunyesha katika sehemu za Ziwa Viktoria, Bonde la Ufa na Kaskazini Mashariki mwa nchi.

Kwa muda wa wiki moja iliyopita, mvua kubwa imeshuhudiwa katika maeneo ya Kaskazini Mashariki mwa Bonde la Ufa na Kati, huku viwango vya joto vikishuka katika sehemu nyingi nchini.

Kaunti za Siaya, Kisumu, Homa Bay, Migori, Kisii, Nyamira, Trans Nzoia, Baringo, Uasin Gishu, Elgeyo Marakwet, Nandi, Laikipia, Nakuru, Narok, Kericho, Bomet, Kakamega, Vihiga, Bungoma na Busia zitashuhudia mvua katika sehemu kadhaa nyakati za asubuhi na manyunyu katika sehemu zingine wakati wa adhuhuri kwa siku saba zijazo.

Kaunti za Nairobi, Nyandarua, Nyeri, Kirinyaga, Murang’a, Kiambu, Meru, Embu na Tharaka Nithi zitashuhudia asubuhi zenye baridi na mawingu mengi.

You can share this post!

Ubadilishaji wa mitungi ya gesi wapigwa marufuku

Wanafunzi wana kiu ya kuelewa mimba, hedhi na magonjwa ya...

adminleo