Makala

TAHARIRI: Tusipuuze kisa cha kijana kuingia Ikulu

June 11th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

NA MHARIRI

TUKIO ambapo mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Jomo Kenyatta alipigwa risasi na kukamatwa kwa kuingia Ikulu bila idhini ya kisheria, inapaswa kuchukuliwa kwa uzito.

Ingawa hii si mara ya kwanza raia wa kawaida kuingia Ikulu jinsi hii, sababu zilizotolewa na mwanachuo huyo Brian Kibet Bera ni za aina yake.

Kwenye visa vichache kama hivyo, ambavyo vimewahi kuripotiwa miaka iliyotangulia, raia waliokamatwa walijitetea kwamba walitaka tu kujionea Ikulu kwa macho, na wengine wakasemekana hawakuwa wenye akili timamu.

Kisa cha Bera ni cha kipekee kwa sababu huyu ni kijana aliyepanga kuingia Ikulu akiwa na lengo la kumdhuru Rais Uhuru Kenyatta.

Maandishi kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Facebook, yalionyesha alikuwa amepanga uvamizi huo kwa muda akidai utawala wa Rais Kenyatta umechangia unyanyasaji na kuongeza umaskini kwa walalahoi, huku mabwenyenye wakifaidika kwa kupora mali ya umma.

Malalamishi kama haya yamekuwa yakienea mno miongoni mwa Wakenya wanapokusanyika katika sehemu tofauti za kijamii, ikiwemo mitandaoni.

Kulikuwa hata na fununu za maandalizi ya mapinduzi ya serikali ambazo zilifanya maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kumkamata mwanaharakati Boniface Mwangi mwezi uliopita.

Ikiwa changamoto za kimaisha ndizo zilimfanya Bera kutatizika kimawazo hadi achukue hatua hiyo, ambayo baadhi wanaona ni ya kijasiri na wengine kusema ni upumbavu, tunafaa tutafakari hali itakuwaje kama kila Mkenya anayepitia hali kama hiyo ataamua kufuata mfano wake.

Hii ni hatari inayotukodolea macho. Tutapotoka kama taifa iwapo tutaamua kuifumbia macho.

Tukumbuke ni nadra kwa taifa, hasa barani Afrika katika enzi hizi, kunufaika kutokana na mapinduzi. Uporaji wa mali ya umma, ulafi na ukwepaji sheria ni miongoni tu mwa tabia mbovu za viongozi, ambazo zimefanya Wakenya wengi kupoteza matumaini maishani.

Hivyo basi viongozi wawe mstari wa mbele kuonyesha mienendo itakayowapa wananchi matumaini ya kuishi maisha bora.