Habari Mseto

Achanganyikiwa kortini kung'amua pingu alizokiri kuiba zimeibwa tena

June 11th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na RICHARD MUNGUTI

KIBARUA aliyekamatwa akiwa na pingu katika soko la Kenyatta karibu na mtaa wa mabanda wa Kibera, Nairobi anakondolewa na kifungo cha miaka mitatu gerezani.

Peter Irungu aliyekiri kupatikana akiwa na pingu, mali ya serikali, alichanganyikiwa kortini kwa muda mrefu alipoulizwa na hakimu mkuu Francis Andayi: “Ulijua pingu ulizokamatwa nazo na polisi zilikuwa zimeibwa?”

“Sikujua kama zimeibwa. Niliziokota tu na nilikuwa nazipeleka kituo cha polisi cha Kilimani nilipokamatwa,” mshtakiwa alijibu.

“Mimi nilikamatwa Juni 7, 2019 na polisi. Sikuziiba pingu hizo. Niliziokota nikiwa na marafiki wengine katika mtaa wa Ngumo,” Bw Irungu alimjibu hakimu.

“Nimekuuliza ikiwa ulijua pingu hizo zilikuwa zimeibwa.”

Hakimu alimweleza mshtakiwa kuwa adhabu ya kupatikana na vifaa vya Serikali ni kifungo cha gerezani miaka mitatu , ama kutozwa faini ama kufanya kazi ya umma katika kampi ya Chifu.

“Nimekusimulia haya ndipo upate ufahamu kuhusu shtaka linalokukabili…” hakimu akamwambia.

“Nami nimekuambia nilikuwa napeleka pingu kituo cha polisi cha Kilimani nilipotiwa nguvuni. Sijui kama zilikuwa zimeibwa ila niliziokota,” mshtakiwa alimjibu.

Mshtakiwa alikiri alipatikana na pingu hizo na kuomba mahakama imsamehe kwa vile hakujua pingu zimeibwa.

Hakimu aliamuru mshtakiwa azuiliwe kuwezesha kiongozi wa mashtaka Bi Kajuju Kirimi kutoa maelezo ya kesi hiyo Jumatano.