Babake mwanafunzi aliyekamatwa akiingia Ikulu adai mwanawe ana matatizo ya kiakili

Na SAMMY WAWERU

BABAKE mwanafunzi aliyekamatwa akiingia Ikulu kinyume cha sheria amesema mwanawe ana matatizo ya kiakili.

David Bera hata hivyo, ameeleza kugutushwa na tukio hilo akisema hakutarajia angefanya jambo la aina hiyo.

Brian Kibet Bera, 25, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT) alikamatwa na polisi kwa kuingia Ikulu ya Nairobi mnamo Jumatatu jioni.

Babake alisema Jumanne mwanawe yuko katika ratiba ya matibabu ili kukabiliana na hali anayopitia.

“Mvulana wangu ana shida za kiakili na anaendelea kupokea matibabu,” alisema.

Akisimulia baadhi ya matukio ya kushangaza aliyofanya awali, Bw David alisema Kibet angemgeuka na hata kumtandika anapomtembelea katika hospitali moja mjini Eldoret ambako hupokea matibabu.

Alisema mwanawe amekuwa na mazoea ya kupotea kiholela na hata kutishia kujitia kitanzi. “Kuna wakati alijaribu kukwea Mlima Kenya kinyume cha sheria, alitiwa nguvuni na nilipoarifiwa sikuwa na budi ila kuenda na kuelezea hali yake afisa mkuu wa polisi kituo alichofungiwa Nyeri. Alielewa na akamuachilia,” alisema.

David ambaye ni mhadhiri katika taasisi moja ya elimu ya juu Eldoret, pia alisema kuna wakati mwanawe alitaka kusafiri Mombasa kwa miguu japo akalemewa alipofika Athi River.

Alisema hali yake ya afya inaendelea kudhoofika akitaja dalili za kupungua kwa kiwango cha kilo.

“Tukio alilofanya ni hatia, ninaamini iwapo angekuwa razini hangefanya hivyo,” alisema.

Bw David alisema hayo katika mahojiano na runinga ya Citizen.

Kulingana na taarifa kutoka kitengo cha mawasiliano afisi ya Rais, PSCU, Brian Kibet Bera, alikwea lango moja Ikulu na alijeruhiwa vibaya kwa kupigwa risasi na polisi wanaoshika doria katika lango hilo alipokaidi amri ya kusalimisha kisu alichokuwa amekibeba.

Mshukiwa alipelekwa katika Kituo cha Polisi cha Kileleshwa na kusajiliwa katika Kitabu cha Matukio nambari 39 kabla ya kupelekwa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) kwa matibabu.

Kumlenga kiongozi

Mwanafunzi huyo wa taaluma ya uhandisi JKUAT, kwenye ukurasa wa akaunti yake ya Facebook kwa muda wa siku kadhaa zilizopita amekuwa akipakia machapisho yanayolenga kiongozi mmoja wa hadhi ya juu nchini akionekana kueleza ‘ghadhabu’ zake.

Babake hata hivyo aliiomba serikali kumsaidia kuimarisha afya yake. “Nimemjua kama mvulana mzuri, akitibiwa arejee hali yake ya kawaida atafanyia taifa hili maendeleo.

“Hana rekodi yoyote ya kushiriki uhalifu, ninaomba serikali inisaidie kumnasua kutoka kwa hali yake kiafya,” aliirai, akiomba Wakenya kuepuka kumkosoa isivyofaa. Wachangiaji mitandaoni wanaendelea kutoa hisia tofauti kuhusiana na tukio hilo.

Uchunguzi wa nia yake kuingia Ikulu unaendelea, na endapo atawasilishwa mahakamani huenda korti ikaagiza afanyiwe uchunguzi wa kiakili kwa kufanya kosa lisilo la kawaida.

Ikulu ni pahali palipotengewa kuwa na ulinzi mkali kwa mujibu wa sheria za maeneo yanayolindwa. Anayenuwia kuingia Ikulu anapaswa kuwa na kibali kutoka kwa asasi husika au maafisa waliojukumika kuruhusu mmoja kuingia.