Matiang'i akutana na jamii za Pokot na Marakwet, azindua eCitizen Nakuru
NA RICHARD MAOSI
Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i Jumatano aliandaa mkutano wa dharura na jamii ya Wapokot na Marakwet, katika ukumbi wa Menengai Social Hall Nakuru, ili kujadili suala la ukosefu wa usalama.
Hafla hiyo iliwaleta pamoja viongozi wa kidini na wazee wa jamii hizo mbili, waliojadili kwa kina kuhusu ongezeko la visa vya uhalifu, huku wakitaka muafaka kupatikana haraka.
Ingawa wanahabari hawakuruhusiwa kuhudhuria hafla hiyo, Dkt Matiang’i aliwahutubia viongozi hao, katika mkutano wa faragha uliochukua saa nzima huku ulinzi mkali ukiimarishwa.
Baadaye alifululiza hadi kwenye Idara ya Uhamiaji mjini Nakuru ambapo alizindua rasmi kituo cha kutoa huduma za eCitizen.
Aliandamana na Mkuu wa Polisi ukanda wa Bonde la Ufa Chimwanga Mwongo, Gavana wa Nakuru Lee Kinyanjui, Kamishna wa Kaunti Erustus Mbui, Mbunge wa Nakuru Mashariki David Gikaria na mbunge wa Nakuru Magharibi Samwel Arama.
Dkt Matiang’i aliwataka raia wasitegemee huduma za kupata visa na pasipoti kupitia kwa watu ambao wanaweza kuwatapeli kwa urahisi.
Aliongezea kuwa pasipoti za zamani zinafaa kufutiliwa mbali, kufikia Septemba mwaka huu, ambapo mfumo mpya wa kujisajili utaanza.
“Watu milioni 2.5 walikuwa wakitumia mfumo wa zamani lakini kufikia sasa, tayari watu milioni 1.5 wamegeukia mfumo wa kisasa,” akasema.
Awali majiji ya Mombasa, Nairobi na Kisumu ndiyo yalikuwa yakitoa huduma hizi, na sasa miji ya Eldoret, Embu, Kisii na Nakuru imejumuishwa.
Aidha majiji ya kigeni kama vile Pretoria, Washington, London, Paris yameorodhodheshwa katika mfumo huu.
Matiang’i alisema kuwa serikali iliacha kutoa vibali kwa raia wa kigeni zamani, na wale wanaotaka kufanya kazi humu nchini wanastahili kutuma maombi wakiwa katika mataifa yao.
“Isipokuwa wale wachache ambao bado wanakaa humu nchini kinyume na sheria, hivi karibuni watanaswa na kurudishwa katika mataifa yao,” akasema.
Aliongezea kuwa wale wachache ambao tayari wamenaswa na serikali wamesafirishwa katika mataifa yao, huku polisi wakijizatiti kuwatimua wengine.
Kwa upande mwingine aliwaonya viongozi kujiepusha na uchochezi dhidi ya wakazi wanaoishi katika mitaa inayopatikana Nakuru.
Akiwahutubia raia katika majengo ya uhamiaji jijini Nakuru, alieleza kuwa ukosefu wa usalama utaathiri uwekezaji hasa wakati huu ambapo kaunti ya Nakuru inakaribia kuwa jiji.
Pia Matiang’i aliendeleza salamu za handisheki na akaungama kumsamehe mbunge wa Nakuru Mashariki David Gikaria kwa kuvunja sheria mapema mwezi uliopita.
Aliwataka viongozi wa ukanda kuketi pamoja na kujadili jinsi ya kukabiliana na magenge yanayoibuka yanayowahangaisha wakazi wa Nakuru.
Mbunge wa Njoro Chjarity Kithambi alisema eCitizen itasaidia kutengeneza nafasi nyingi za ajira miongoni mwa vijana na kuwapunguzia raia mzigo mzito wa kusafiri hadi Nairobi kila mara kutafuta huduma hizi.
“Kwa mfano wagonjwa wanaotafuta matibabu katika mataifa ya nje kama vile India hawatacheleweshwa wakisubiri kuhudumiwa,” Bi Charity alisema.