• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 9:50 AM
Familia 30 zakosa makao kufuatia mafuriko Nyando

Familia 30 zakosa makao kufuatia mafuriko Nyando

Na DUNCAN OKOTH

FAMILIA 30 katika kata ndogo ya Kakola Ombaka, eneo bunge la Nyando, Kaunti ya Kisumu zimeachwa bila makao baada ya nyumba zao kufurika maji kufuatia mvua kubwa iliyonyesha eneo hilo na kusababisha mto Nyando kuvunja kingo zake.

Wakazi sasa wanahofia hasara zaidi mafuriko yakiendelea huku watu 300 wakikabiliwa na hatari ya kukosa makao. Tayari, mimea na mali imeharibiwa kufuatia mafuriko hayo yaliyoanza Jumapili usiku baada ya mvua kubwa kuponda eneo hilo wikendi.

Mvua ikiendelea kunyesha, masomo yataathiriwa kwa sababu wanafunzi hawataweza kufika shuleni. “Watu zaidi wanaweza kuathiriwa siku zijazo na watalazimika kuhamia shule nyingine na makanisani,” alisema Bw Sylvan Oyugi.

“Mafuriko yameathiri mimea kama mahindi, mtama na mboga kwenye mashamba yetu,” aliongeza mkazi huyo.

Chifu wa eneo hilo Bw Jacob Ongudi, hata hivyo alisema hakuna vifo vilivyoripotiwa au mifugo kusombwa na mafuriko. Hata hivyo alieleza hofu kwamba hali inaweza kuwa mbaya zaidi.

Mafuriko pia huwa yanaathiri shughuli za biashara eneo hilo kwa sababu huwa ni vigumu kwa wafanyabiashara na wateja kufika soko la karibu la Ahero. Wakazi wanaomba serikali ijenge vizuizi kwenye mto Nyando ili kuzuia maafa.

Walisema kwamba wamejaribu kujenga mahandaki kadhaa lakini juhudi zao hazijafaulu kwa kukosa pesa.

“Tunaomba serikali kujenga vizuizi kwenye mto Nyando na mito mingine,” alisema Bw John Otieno. Mto Nyando huwa unafurika maji kila msimu wa mvua. Kulingana na wakazi, mto huo huwa unafurika maji mara mbili kwa mwaka. Hata hivyo, mwaka huu ilikuwa afueni kwa wakazi mvua ilipochelewa.

Wakazi wanasema wito wao kwa serikali kuwajengea mahandaki umepuuzwa na inachofanya ni kuwapa misaada ya chakula wanapopatwa na janga. Wakati huo huo, ofisi ya idara ya mipango maalumu na mikasa katika Kaunti ya Kisumu imeomba pesa zaidi kutoka kwa serikali kuu iweze kukabiliana na janga la mafuriko katika kaunti hiyo.

Mkurugenzi wa mipango maalumu Bi Ruth Odinga alisema uhaba wa pesa umelemaza juhudi za idara hiyo kutafuta suluhu la kudumu kwa baadhi ya majanga yanayokumbwa wakazi.

“Ili suluhu la kudumu liweze kupatikana, pesa nyingi zinahitajika ambazo hatuwezi kupata kama idara. Serikali ya kitaifa inapaswa kutusaidia kumaliza baadhi ya majanga haya,” alisema Bi Ruth Odinga.

Aliomba serikali ya kitaifa na ya kaunti kushirikiana kuhakikisha zimetengea idara ya mipango maalumu na majanga pesa zaidi katika bajeti ya mwaka ujao.

Kulingana na Bi Odinga, ofisi yake imekuwa ikikabiliana na baadhi ya majanga kwa kujenga mabwawa na mitaro. “Tulijenga mitaro mingi maeneo la Kakola, Mikombe, Oyare na Onyiko. Tangu wakati huo, visa vya mafuriko vimepungua kaunti ya Kisumu,” alisema.

You can share this post!

Aliyenaswa na pingu akiwa mlevi asukumwa rumande

Uavyaji mimba utasalia kuwa hatia – Mahakama

adminleo