• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 7:55 AM
Babake aliyeingia Ikulu aililia serikali impe mwanawe nafasi maishani

Babake aliyeingia Ikulu aililia serikali impe mwanawe nafasi maishani

Na VALENTINE OBARA

BABAKE Brian Kibet Bera, kijana aliyeingia Ikulu ya Nairobi mnamo Jumatatu jioni akiwa na nia ya kumuua Rais Uhuru Kenyatta, amemwomba rais aingilie kati ili kijana huyo aruhusiwe kukamilisha masomo yake.

Bw David Bera amesema mwanawe alikuwa na matatizo ya kiakili kwa karibu miaka miwili sasa, na alipokea matibabu katika hospitali mbalimbali nchini.

“Anaweza kuchangia pakubwa katika nchi hii akipewa nafasi. Kama ataruhusiwa kukamilisha kozi yake ambayo inaisha Julai, anaweza kusaidia nchi hii baadaye. Anahitaji tu matibabu,” akasema Bw Bera alipohojiwa kwenye Runinga ya Citizen mnamo Jumanne usiku.

Brian, 25, alipigwa risasi akajeruhiwa begani na walinzi alipovamia Ikulu mnamo Jumatatu jioni akiwa amejihami kwa kisu.

Awali alikuwa ametishia kwenye mtandao wa Facebook kwa karibu wiki moja kwamba alitaka kumuua Rais Kenyatta akimlaumu kwa kusababisha mateso na unyanyasaji wa walalahoi.

Lakini kwenye mahojiano, babake alisema kijana huyo, ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa tano anayesomea uhandisi katika Chuo Kikuu cha Jomo Kenyatta (JKUAT), ni mwenye nidhamu ya hali ya juu na hangefanya shambulio hilo kama angekuwa mwenye akili timamu.

Vilevile, aliomba vijana wanaoshabikia kitendo hicho mitandaoni wakome na waelewe kwamba mwanawe hakujua alichokuwa akifanya.

“Kile alichofanya hakikuwa sawa na hakuwa mzima kiakili. Kama angekuwa na sawa kiakili hangefanya hivyo. Vijana wasisifu kile alichofanya. Mwanangu ni mgonjwa,” akasema.

Kulingana naye, nidhamu ya Brian ndiyo ilimwezesha kufanya vyema kwenye masomo yake tangu shule ya msingi hadi akapata alama ya ‘A’ kwenye Mtihani wa Kitaifa wa Shule ya Upili (KCSE) na hatimaye kwenda kusomea uhandisi.

Alianza kutatizika kiakili alipokuwa katika mwaka wa tatu chuoni, kulingana na babake.

Katika maandishi yake kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook, Brian alikuwa amekashifu vikali watu wanaodai kwamba amerukwa akili.

You can share this post!

Uavyaji mimba utasalia kuwa hatia – Mahakama

Sitaogopa kuwakamata wanasiasa wachochezi –...

adminleo