• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 8:12 PM
Makamishna IEBC wawe watano, Chebukati aunga

Makamishna IEBC wawe watano, Chebukati aunga

Na CHARLES WASONGA

MWENYEKITI wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati sasa anakubaliana na wabunge kwamba idadi ya makamishna wa tume hiyo inafaa kupunguzwa kutoka saba hadi watano, ili kuimarisha utendakazi wake.

Hata hivyo, Bw Chebukati ametofautiana na msimamo wa wabunge wanachama cha Kamati kuhusu Haki na Masuala ya Sheria (JLAC) kwamba tume hiyo haijaundwa kikatiba kwa kuwa na makamishna watatu baada ya makamishna wanne kujiuzulu.

“Ilivyo sasa tunaendesha shughuli za tume kihalali kwa mujibu wa Katiba hata ingawa sisi ni makamishna watatu pekee; na licha ya hitaji la sheria ya IEBC kwamba kunahitajika angalau makamishna watano. Hata hivyo, nakubaliana na pendekezo la mswada wa marekebisho ya sheria kwamba tume hii iwe na makamishna watano badala ya saba ilivyo sasa,” akasema.

Bw Chebukati alisema hayo jana katika majengo ya bunge alipowasilisha mapendekezo ya tume hiyo kuhusu mswada wa marekebisho ya sheria ya IEBC inayoshughulikiwa na kamati ya JLAC inayoongozwa na Mbunge wa Baringo Kaskazini Bw William Cheptumo.

Alieleza wanachama wa kamati hiyo kwamba kulingana na katiba ya sasa, tume za kikatiba zinapaswa kuwa na idadi ya wanachama wasiopungua watatu na wasizidi tisa.

“Hii ndio sababu katika kesi tatu zilizowasilishwa mahakamani kupinga uhalali wa IEBC baada ya wenzetu wanne kujiuzulu, mahakama kuu iliamua kwamba tume hii ilivyo sasa inaafiki hitaji la katiba kimuundo,” akasema.

“Tulivyo watatu, sisi hukutana na kupitisha maamuzi haraka. Kwa hivyo, tumeweza kutekeleza majukumu yetu yote 11 kwa mujibu wa Katiba ya sasa,” akasema.

Alikuwa akiwajibu Mbw Cheptumo, Peter Kaluma (Homa Bay Mjini), Olago Aluoch (Kisumu Mashariki) na Anthony Kiai walioshikilia kuwa tume hiyo haiwezi kupitisha maamuzi makuu ya kisera kwa kuwa na makamishna watatu pekee.

“Kama kamati hatujashawishika kuwa kama tume hii inaweza pia kutekeleza majukumu mazito yaliyoko mbele yale wakati huu kama uainishaji wa mipaka na hata kura ya maamuzi,” Cheptumo akasema.

Makamishna wa IEBC waliojiuzulu mwaka jana ni; aliyekuwa naibu mwenyekiti Bi Connie Maina na makamishna Dkt Paul Kurgat na Margaret Mwanjala. Naye Dkt Roselyn Akombe alijiondoa mnamo Oktoba 20, 2017, kabla ya uchaguzi wa marudio ya urais.

Bw Chebukati pia anapendekeza kuwa mamlaka ya Rais ya kuteua mwenyekiti wa tume hiyo yadhibitiwe kupitia mabadilisho ya sheria ili jopo la uteuzi liwe likiwasilisha jina moja pekee kwake kwa uteuzi badala ya majina mawili inavyofanyika sasa.

You can share this post!

Mgao kwa sekta ya kilimo wadidimia

IEBC kuwahoji 10 kwa wadhifa wa afisa mkuu

adminleo