• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 11:38 AM
JAMVI: Echesa azinduka, ajipanga kwa kura za 2022

JAMVI: Echesa azinduka, ajipanga kwa kura za 2022

Na BENSON MATHEKA

Tangazo la aliyekuwa Waziri wa Michezo, Bw Rashid Echesa kwamba atamuunga kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC) kwenye uchaguzi mkuu wa 2022 ni hatua ya kukumbatia eneo na jamii analotoka huku akimezea mate kiti cha uongozi.

Wadadisi wanasema Bw Echesa ambaye amekuwa akimuunga mkono Naibu Rais William Ruto, amegutuka kwa wakati ufaao na kukumbatia watu wa nyumbani ili kuimarisha nafasi yake ya kushinda kiti anachopanga kugombea mwaka wa 2022.

Wachanganuzi wanasema ni hatua nzuri ambayo Bw Mudavadi anafaa kuchukua kuimarisha ngome yake ya kisiasa eneo la Magharibi mwa Kenya ikizingatiwa kuwa Bw Echesa ni mmoja wa viongozi vijana wenye ushawishi mashinani.

Hata hivyo, wanamuonya kuwa mwangalifu na wanasiasa wanaojitokeza kushirikiana naye akisema wanaweza kutumiwa na washindani wake kumharibia nafasi ya kushinda urais.

“Inaweza kuwa hatua nzuri iwapo Mudavadi ataitumia kuimarisha ngome yake kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022. Hata hivyo anafaa kuwa mwangalifu zaidi ili wanasiasa wanaojitokeza kumuunga mkono wasiwe wametumwa kuvuruga azima yake ya kuwa rais,” asema mchanganuzi wa siasa Ambrose Weda.

Mwishoni mwa wiki jana, Bw Echesa alimruka Naibu Rais William Ruto na kusema kwamba atamuunga mkono Bw Mudavadi kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Akizungumza katika hafla ya mazishi ambayo Bw Mudavadi alihudhuria, Bw Echesa alimtaka kiongozi huyo wa chama cha ANC kuleta pamoja viongozi wa jamii ya Waluhya ili kupiga jeki azima yake ya kuwa rais.

“Wale walio katika chama cha ANC wanafaa kufahamu kwamba Bw Mudavadi ndiye mgombea urais maarufu eneo la Magharibi na ni lazima tumsaidie apate kiti hicho kwa njia zote,” alisema Bw Echesa.

Ili kudhihirisha kwamba alikuwa ameamua kumuunga Bw Mudavadi, Bw Echesa alisema atatumia rasilmali zake kumpigia debe makamu huyo wa rais wa zamani kuhakikisha jamii ya Mulembe itatoa rais wa tano wa Kenya.

“Ninamhimiza Bw Mudavadi kuwa jasiri na kuanza kuunganisha eneo letu lote kwa sababu ndiye kiongozi maarufu zaidi eneo la Magharibi,” aliongeza Bw Echesa na kuonya kuwa kuna wanasiasa wa eneo hilo wanaotumiwa kumharibia Mudavadi nafasi ya kuwa rais.

Wanasiasa wengine kutoka jamii ya Mulembe ambao wametangaza azima yao ya kugombea urais ni Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya wa chama cha ODM na Moses Wetangula wa chama cha Ford Kenya.

Kulingana na Bw Echesa baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakimuumbua Bw Mudavadi kupitia kura ya maoni walizofadhili ili kuzima nafasi yake ya kuwa rais.

Lakini wadadisi wanasema Bw Echesa anaweza kutumiwa na Bw Ruto ambaye amekuwa akijaribu kupenya eneo la Magharibi kupitia wanasiasa wanaomuunga mkono.

“Bw Echesa anaweza kutangaza hadharani na kumpamba Bw Mudavadi na sifa za kila aina lakini swali ni je, huu ndio wakati ametambua ana sifa hizo?” anahoji Bw David Wanyama, mdadisi wa siasa.

Anasema umaarufu wa Bw Mudavadi katika ngome yake hauwezi kupiku wa kiongozi wa upinzani Raila Odinga ambaye amekuwa akipata kura nyingi. Kwenye uchaguzi wa 2013 Bw Odinga alipata kura nyingi eneo la Magharibi kuliko alizopata Mudavadi ambaye pia aliwania urais.

Kulingana na Bw Echesa, jamii ya Mulembe ni lazima iwe katika serikali ijayo ikiongozwa na Bw Mudavadi.

“Ni mwangaza gani ambao Bw Echesa ameona hadi akamkumbatia Mudavadi na kumruka Bw Ruto ambaye alimfanya kuonja uwaziri kwa mwaka mmoja? Hili ndilo swali ambalo wandani na wanamikakati wa Bw Mudavadi wanafaa kujiuliza,” asema Bw Wanyama.

Mdadisi huyo anasema hatua ya Bw Echesa inaweza kuibua mwamko mpya wa kisiasa eneo la Magharibi hasa baada ya kuzika tofauti zake na Seneta wa kaunti ya Kakamega Cleophas Malala.

Kulingana na Bw Malala, yeye na Bw Echesa wamekubaliana kuunga mtu kutoka jamii ya Mulembe kugombea urais.

“Kumbuka Bw Malala amekuwa muasi katika chama cha ANC kilichomfadhili bungeni kwa kumuunga Bw Odinga badala ya kuelekeza uaminifu wake kwa Bw Mudavadi. Kwamba ameungana na Echesa aliyekuwa mshirika wa Bw Ruto na kuapa kumuunga Mudavadi, kuna uwezekano wa mwamko mpya eneo la Magharibi,” alisema Bw Wanyama.

Kulingana na Bw Malala, viongozi vijana kutoka jamii ya Mulembe wanataka kufuta dhana kwamba hawamheshimu Bw Mudavadi kwa kumuunga mkono.

Akizungumza katika kituo kimoja cha redio mapema wiki hii, Bw Weda alitilia shaka uaminifu wa wanasaisa wanaojitokeza kumuunga Bw Mudavadi akidai wanaweza kuyumbisha azima yake ya kuwa rais.

Mdadisi wa siasa za Magharibi ya Kenya Ezra Makokha anasema kwamba kuna wanasiasa wasioweza kumfaidi Bw Mudavadi.

Alitaja Bw Echesa na Bw Malala kama wanasiasa wasiokuwa na misimamo thabiti ya kisiasa.

“Nafikiri lengo la wanasiasa hao ni kutumia jina la Mudavadi kutimiza malengo mengine ya kibinafsi yao na washirika wao. Kumbuka Malala aliasi msimamo wa chama cha Mudavadi na kuegemea upande wa Bw Odinga,” asema.

You can share this post!

‘Kijana fupi nono round’ akataa kazi ya Ruto

TAHARIRI: Kisa cha Sharon na Melon kiwe funzo

adminleo