• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 9:55 AM
Mvua kubwa kunyesha katika kaunti nyingi

Mvua kubwa kunyesha katika kaunti nyingi

Na COLLINS OMULO

IDARA ya utabiri wa hali ya hewa nchini imetoa ilani kwa Wakenya wajiandae kwa mvua kubwa katika baadhi ya maeneo nchini kwa siku tano zijazo kuanzia Jumatatu.

Mkurugenzi wa idara hiyo, Bw Peter Ambenje, alisema maeneo mengi ya nchi yatashuhudia ongezeko la mvua katika kipindi hicho.

“Mvua kubwa inatarajiwa kuanzia leo katika maeneo ya Magharibi, Kusini na Katikati mwa Rift Valley, na eneo la kati mwa Kenya ikiwemo Nairobi. Hata hivyo mvua hiyo haitakuwa kubwa kama ilivyoshuhudiwa hivi majuzi,” akasema Bw Ambenje.

Aliongeza kuwa mvua hiyo huenda itaendelea kunyesha hadi Jumatano katika kaunti zilizo kusini mwa Rift Valley, nyanda za chini za Kusini Mashariki, Kaskazini na maeneo ya kati ikiwemo Nairobi.

Kaunti za Kisii, Kericho, Bomet, Narok, Migori, Kakamega, Kajiado, Nakuru, Kwale, Marsabit, Wajir, Isiolo, Turkana, Samburu, Nairobi, Nyeri, Kiambu, Muranga, Kitui, Machakos, Makueni, Kwale, Kilifi, Mombasa, Lamu na Taita Taveta ni miongoni mwa zile ambazo zitapata na mvua kubwa.

Idara hiyo ilionya wakazi wa mijini wajihadhari na mafuriko ya ghafla kwani huenda kukawa na mafuriko katika maeneo ambapo hakujanyesha sana kufikia sasa, na wakazi wametakiwa wakae katika maeneo salama hadi mafuriko yapungue.

“Msitembee wala kuendesha magari kwenye mafuriko. Endeleeni kusikiliza vyombo vya habari ambapo matangazo kuhusu hali ya hewa yataendelea kutolewa kadri na jinsi hali inavyobadilika. Zaidi ya hayo, ilani zitatolewa tukiendelea kutathmini hali hii,” akasema Bw Ambenje.

Kulingana na utabiri huo wa siku tano kuhusu hali ya hewa kati ya Machi 10 hadi Machi 14, kaunti zilizopakana na Ziwa Victoria ikiwemo Siaya, Kisumu, Homa Bay na Migori zitashuhudia vipindi vya jua asubuhi na kufuatwa na mvua na ngurumo za radi katika maeneo kadhaa mchana.

Hali kama hii itashuhudiwa pia katika kaunti za Kisii, Nyamira, Trans Nzoia, Baringo, Uasin Gishu, Elgeyo-Marakwet, Nandi, Laikipia, Nakuru, Narok, Kajiado, Kericho, Bomet, Kakamega, Vihiga, Bungoma na Busia lakini mvua kubwa zaidi itanyesha Kusini mwa Rift Valley hasa Narok kesho na Jumatano.

Kaunti za nyanda za juu za kati mwa Kenya kama vile Nairobi, Nyandarua, Nyeri, Kirinyaga, Murang’a, Kiambu, Meru, Embu na Tharaka Nithi zinatarajiwa kupokea mvua asubuhi kuanzia kesho hadi mwishoni mwa kipindi hicho cha utabiri.

Maeneo ya nyanda za chini za Kusini Mashariki ikiwemo kaunti za Kitui, Makueni, Machakos na Taita Taveta pia yatapokea mvua asubuhi na mchana katika maeneo kadhaa kuanzia Jumatano.

Hata hivyo, kutakuwa na vipindi vya jua katika kaunti za Kaskazini Magharibi, Pwani na Kaskazini Mashariki.

You can share this post!

Wakenya Maritim na Chebitok watawala Barcelona Marathon

Wasahihishaji wa KCSE waikejeli KNEC kutowalipa hela za 2017

adminleo