Habari MsetoSiasa

Awarai Wameru kumpa Ruto kura zao zote 2022

June 18th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na Charles Wanyoro

SENETA wa Meru Mithika Linturi ameitaka jamii ya Wameru imuunge mkono Naibu Rais William Ruto katika kinyang’anyiro cha urais 2022.

Bw Linturi aliyekuwa ameandamana na mbunge wa Tigania Mashariki Josphat Gichunge alisema kuwa jamii ya Wameru itatimiza ahadi Rais Uhuru Kenyatta alitoa kwa naibu wake Dkt Ruto kabla ya uchaguzi wa 2013 na 2017 kwamba atamuunga mkono baada ya kukamilisha mihula yake miwili.

“Rafiki yetu Rais Kenyatta hatawania tena kwa sababu sheria haimruhusu. Awali kulikuwa na makubaliano angeunga mkono Ruto baada ya kukamilisha kipindi chake, tusimkimbie wakati huu ambapo anatuhitaji,” akasema Bw Linturi.

Bw Gichunge alisema jamii wa Wameru itanufaika zaidi chini ya uongozi wa Dkt Ruto kwani tayari amezindua miradi kadhaa katika eneo hilo.

Wakati huo huo, Bw Linturi ambaye ni naibu mwenyekiti wa Kamati ya Masuala ya Sheria na Haki za Binadamu katika Seneti, alisema bunge linalenga kufanyia marekebisho sheria za uchaguzi ili kuzuia ghasia za baada ya uchaguzi ambazo hushuhudiwa kila baada ya miaka mitano.