• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
‘Referenda yafaa kujali maslahi ya wananchi, si matakwa ya viongozi walafi’

‘Referenda yafaa kujali maslahi ya wananchi, si matakwa ya viongozi walafi’

Na DERICK LUVEGA

KIONGOZI wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi ametofautiana na wabunge wa ODM kuhusu wito wa kutaka kufanyika kwa kura ya maamuzi ili kubadili muundo wa serikali kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2022.

Akizungumza Jumapili katika Kanisa la Apostolic Pentecostal Evangelism (Apec) katika eneobunge la Hamisi, Kaunti ya Vihiga, Bw Mudavadi alisema kura ya maamuzi inafaa kuandaliwa ili kushughulikia maslahi ya wananchi wa kawaida na wala si matakwa ya watu binafsi.

Bw Mudavadi alihoji ni kwa nini wanasiasa wamekuwa wakitaka kufanyika kwa kura ya maamuzi bila kuwaambia wananchi mambo wanayotaka yabadilishwe.

Wiki iliyopita, wabunge wa ODM walimtaka Waziri wa Fedha Henry Rotich kutenga fedha zitakazotumiwa kuandaa kura ya maamuzi.

Wabunge wa ODM, haswa kutoka Nyanza, walisisitiza kuwa kura ya maamuzi ndiyo itadhihirisha kuwa kumbe Rais Kenyatta yuko tayari kuunganisha nchi kupitia handisheki baina yake na kiongozi wao Bw Raila Odinga.

Lakini Bw Mudavadi aliyekuwa akiongoza hafla ya kuchangisha fedha kwa ajili ya kanisa la Apec alipuuzilia mbali wito huo.

“Kumekuwa na ongezeko la kutaka kuwepo kwa kura ya maamuzi. Baadhi ya viongozi wametaka wanasiasa kutangaza msimamo ikiwa wanaunga au kupinga mabadiliko ya katiba. Lakini swali ni je, wanataka kubadilisha nini?” akauliza Bw Mudavadi.

Akaendelea: “Hadi tujue wanacholenga kubadilisha ndipo tutatangaza msimamo ikiwa tunaunga au kupinga.”

“Tunafaa kuwashirikisha wananchi katika suala hili la kura ya maamuzi lisiwe la viongozi wachache tu. Ikiwa tunalenga kugawanya nafasi za uongozi, wananchi watapata nini?” akasema Bw Mudavadi.

Wakati huo huo, kiongozi wa ANC alimtaka Rais Kenyatta kukaza kamba kuhakikisha kuwa anaangamiza zimwi la ufisadi.

Alionya kuwa wanasiasa walio katika kundi la Tanga Tanga linalounga mkono Naibu wa Rais William Ruto, wanachafua sifa zao kwani wamekuwa wakihusishwa na visa vya ufisadi.

“Kundi la Tanga Tanga limekuwa likihusishwa na ufisadi. Sifa ya kundi hilo ni mbaya na huenda wanasiasa hao wakajichimbia kaburi la kisiasa,” akasema Bw Mudavadi.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Naibu Gavana wa Vihiga Dkt Patrick Saisi, Mwakilishi wa Wanawake wa Vihiga Beatrice Adagala na mwenyekiti wa kitaifa wa ANC Kevin Lunani.

Dkt Patrick Saisi (ODM) hata hivyo alimtaka Bw Mudavadi kukoma kushambulia Bw Odinga huku akisema kuwa hataweza kuingia ikulu bila Baraka za kinara wa ODM.

“Mudavadi anafaa kushirikiana na Raila Odinga kwa sababu ni wewe (Mudavadi) anayeweza kunufaika. Usiwahi kupigana kisiasa na Raila,” akasema.

You can share this post!

Pendekezo la Rotich kuhusu bodaboda lazidi kupingwa

Vijana wapendekeza wafundishwe kuhusu ngono na uzazi

adminleo