TAHARIRI: Rais ana haki ya kukemea viongozi
NA MHARIRI
SIKU ya Jumapili, Rais Uhuru Kenyatta awakemea hadharani wanasiasa ambao wamejihusisha na kampeni za mwaka 2022, ilhali kumebaki miaka mitatu ya kuwafanyia kazi wananchi.
Akionekana mwenye hasira, Rais aliwataka wanasiasa wanaozurura kila pembe ya nchi wakitangaza sera zao, wakome mara moja.
Jana wanasiasa kadhaa wa eneo la Mlima Kenya walijitokeza na kumkosoa Rais wakidai alitumia lugha iliyowadunisha. Walidai kuwaita “mikora” na majina mengine kuliwadhalilisha kama viongozi waliochaguliwa kuwakilisha wananchi mashinani.
Kinachojitokeza ni kwamba maneno hayo yanatumika vyema katika lugha ya Kiswahili kueleza tabia za wahusika. Kwa mfano ni ukora kwa mwanasiasa kuanza kuwatangazia wananchi kuwa atafanya hivi au vile akichaguliwa mwaka 2022, ilhali sasa hivi kuna ahadi alizotoa mwaka 2017 na hajaanza kuzitimiza.
Wanasiasa waliomlaumu Rais Kenyatta walidai kuwa wamejiunga na kundi la Tanga Tanga kwa sababu Naibu wa Rais Dkt William Ruto amekuwa akiwaunga mkono katia Harambee wanazofanya kila wikendi. Swali wanalofaa kujiuliza ni ikiwa Harambee ni halali au la.
Suala lililo muhimu ni ujumbe alioutoa wakati wa hotuba yake katika eneo la Kasarani, Nairobi na wala si jinsi alivyoutoa ujumbe huo.
Anachotaka ni viongozi wote washirikiane kutimiza Ajenda Kuu Nne ambazo serikali imejiwekea. Kufikia sasa, hakuna juhudi zozote kutoka kwa wanasiasa kuunga mkono ajenda hizo, ambazo zikianza kutekelezwa zitasaidia nchi kufikia Ruwaza ya mwaka 2030.
Isitoshe, viongozi hao walipopigiwa kura walipewa pesa za hazina ya Maendeleo katika maeneo bunge yao. Kama viongozi wazuri, wangekuwa wanawashirikisha wananchi kubuni sera au kuendeleza miradi ya kuwanufaisha. Kwa mfano, kuanzisha kiwanda cha majani chai au kahawa ambapo vijana wengi watapata ajira, ni bora zaidi kuliko kuchanga mamilioni kwa kanisa.
Hakuna anayemkataza mtu yeyote kuwania wadhifa wowote wa kisiasa mwaka 2022. Kila ambacho Rais Kenyatta na Wakenya wengi wanapinga, ni kuendeleza kampeni ilhali kuna manifesto ambayo viongozi wa chama cha Jubilee waliahidi kutekeleza.
Uasi huu wa wazi dhidi ya Rais ni mfano mbaya, na hatari kwa udhbiti wa kisiasa. Itambuliwe kuwa Katiba inamtaja Rais kuwa kiunganishi kwa umoja wa nchi. Tusipolinda hadhi ya urais, basi siku za usoni huenda wadhifa huo ukapoteza umuhimu wake.