• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Mkutano wa Uhuru na Raila wazidi kusifiwa

Mkutano wa Uhuru na Raila wazidi kusifiwa

Na WAANDISHI WETU

VIONGOZI na makundi mbalimbali wameendelea kupongeza hatua ya kinara wa NASA Raila Odinga na rais Uhuru Kenyatta kukutana.

Wa punde zaidi ni viongozi wa baraza la jami ya Luo, waliosema hatua hiyo italeta maridhiano ya kweli nchini.

Mwenyekiti wa baraza hilo, Ker Willis Opiyo Otondi, alisema Jumapili katika ukumbi wa Ofafa Memorial mjini Kisumu, kwamba mkutano huo utawezesha kuwepo maridhiano ya kitaifa ambayo yatawezesha kupatikana kwa ustawi wa uchumi, na kuimarika kwa nchi kisiasa na kijamii.

“Sisi kama wazee wa jamii, tumejitolea kuendeleza na kuunga mkono hoja tisa ambazo viongozi hao wawili walikubaliana, kama kigezo na dira ya mazungumzo zaidi,” alisema Bw Otondi kwenye taarifa aliyoitia saini, pamoja na katibu wa baraza hilo Mzee Adera Osawa na Mchungaji Stephen Omondi Oludhe.

Nacho chama cha Kanu kilisema mkutano huo utaunganisha nchi.

Kupitia habari iliyotumwa na mwenyekiti wake, Seneta wa Baringo Gideon Moi, mkutano wa viongozi hao wawili na hatua ya kuhutubia taifa kwa pamoja kuhusu haja ya kuzika siasa na kuanza kuunganisha na kujenga taifa ndiyo dawa mjarabu iliyosubiriwa kuponya taifa kutokana na vidonda vya kisiasa.

“Ujumbe wao utasaidia kuponya vidonda vya kisiasa nchini ili Wakenya waweze kusonga mbele wakiwa kitu kimoja,” akasema Bw Moi.

Chama hicho kiliendelea kumpongeza Rais Kenyatta kwa kutimiza ahadi yake ya kuongoza katika kuleta uwiano wa kitaifa na kuponya nchi ili kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

“Umoja wa kitaifa ni muhimu ili kuelekeza taifa katika maendeleo kwa kuendeleza amani na upendo. Wakati watu wameungana, wanaweza kujinyanyua na kujenga taifa kwa pamoja,” akasema seneta huyo.

Bw Moi alisema chama chake kinatoa ‘uungaji mkono bila masharti’ kwa juhudi hizo ambazo zinalenga kuleta pamoja Wakenya wa kutoka nyanja tofauti, bila kuangalia mirengo ya kisiasa.

“Ni maombi yetu kuwa njia ambayo Rais na kiongozi wa upinzani wamechukua itaelekeza nchi kwa uzalendo upya kwani nchi iliyogawanyika haiwezi kuendelea,” akasema Bw Moi.

Mjini Mombasa, wabunge Aisha Jumwa (Malindi), Owen Baya (Kilifi Kaskazini) na kiongozi wa walio wengi katika bunge la kaunti ya Kilifi Bw Sammy Ndago, walipongeza hatua ya Raila.

Hata hivyo mbunge wa Magarini Bw Michael Kingi alitofautiana nao na kudai kwamba Raila alifaa kushauri wenzake.

Siku ya Jumamosi kinara wa chama cha Amani National Congress (ANC) alisisitza kwamba mkataba kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga hauhusiani kivyovyote na muungano wa Nasa.

Aidha Bw Mudavadi alisema kuwa mkataba huo ni wa watu wawili pekee na sio picha kamili ya mageuzi ambayo Nasa imekuwa ikipigania.

Ripoti za JUSTUS OCHIENG, PETER MBURU na KAZUNGU SAMUEL

You can share this post!

BODABODA: Kizingiti kikuu cha hali ya usalama nchini

Wakazi Mlima Elgon wataka kafyu ya siku 90 iondolewe

adminleo