• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 4:36 PM
Mbunge ashauri KWS kuajiri wawindaji haramu, eti wana ujuzi!

Mbunge ashauri KWS kuajiri wawindaji haramu, eti wana ujuzi!

Na PETER MBURU

MBUNGE wa Mwatate Andrew Mwadime amependekezea Shirika la Uhifadhi wa Wanyamapori (KWS) liwe likiajiri wawindaji haramu kulisaidia kulinda wanyama, akisema ndio wana ujuzi unaofaa kufanya kazi hiyo.

Bw Mwadime ambaye alikuwa akizungumza wakati Waziri Msaidizi wa Utalii Joseph Boinnet na Mkurugenzi Mkuu wa KWS John Waweru walifika mbele ya Kamati ya Bunge Kuhusu Utalii alisema kuwa mbinu ambazo KWS imekuwa ikitumia kuhakikisha kuwa wanyama wanalindwa hazijazaa matunda.

Alisema kama mtu ambaye alikuwa mwindaji haramu utotoni kutokana na mazingira ambapo amelelewa, anafahamu vyema kuwa serikali ikiamua kuwapa kazi vijana wanaoua wanyama wataisaidia kuhakikisha visa hivyo vinakomeshwa, na kumaliza mizozo baina ya wanyama na binadamu.

“KWS iajiri wawindaji haramu kwani ndio wataisaidia kulinda wanyama. Ni mbinu thabiti sana ambayo itazaa matunda,” akasema Bw Mwadime.

Alisema kuwa alishauri shirika hilo hivyo muhula wa ubunge uliopita lakini halikutii ushauri wake, akisema huenda kungekuwa kumeshuhudiwa kupungua kwa visa vya mizozo baina ya wakazi wanaoishi karibu na mbuga na wanyama pori.

Ushauri wake uliungwa mkono na mbunge wa Kajiado Mashariki Peris Tobiko ambaye alilalamika kuwa watu wanaofanya maamuzi katika shirika la KWS hawana ujuzi wowote kuhusu jinsi ya kuishi na wanyama, ilhali maamuzi yao yanaathiri Wakenya wengi.

“Sasa ikiwa watu ambao hawajawahi kuishi na ndege pekee, hata si ndovu, ndio wanafanya maamuzi kuhusu sera za KWS…hii haifai,” akasema Bi Tobiko.

You can share this post!

IEBC isalie na makamishna saba, KNHRC yapendekeza

Mapolo wasaka mwizi wa asali

adminleo