• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 5:55 AM
Mshukiwa wa wizi Zimmerman anusurika kifo

Mshukiwa wa wizi Zimmerman anusurika kifo

Na SAMMY WAWERU

MWANAMUME mshukiwa wa wizi eneo la Zimmerman, Nairobi, Jumanne jioni aliponea tundu la sindano kuuawa na umma wenye ghadhabu.

Mwanamume huyo aliyetaja jina moja tu kwamba anaitwa Roy, inadaiwa kwa ushirikiano na wanaume wengine wawili walivunja nyumba ya mkazi na kujaribu kuiba mali yenye thamani ya pesa kiasi kikubwa.

Taifa Leo imearifiwa kwamba mmiliki ambaye ni mfanyabiashara eneo hilo, alifahamishwa kuhusu jaribio hilo la wizi akafika upesi na kufumania mwanamume huyo akipakia vitu.

“Wenzake waliponyoka, njama yao ilipotibuka. Huyu tulimkamata wakati akijaribu kutoroka,” alisema mfanyabiashara huyo.

Inadaiwa walikuwa wamepakia runinga, mitungi ya gesi na bidhaa zingine zenye thamani ya pesa.

Umati wa watu uliojitokeza, kwa ghadhabu ulimtia adabu mshukiwa huyo japo akanusurika kifo baada ya baadhi ya wakazi kumuokoa.

Alifikishwa katika kituo cha polisi cha askari tawala, AP, kilichoko Zimmerman, Kasarani, ambapo afisa anayesimamia kituo hicho aliagiza apelekwe hospitalini ili kupokea matibabu.

Mshukiwa huyo aliyekiri kushiriki wizi, alidai ni mkazi wa mtaa wa Umoja. Hakuwa na stakabadhi zozote kama vile kitambulisho cha kitaifa.

Baadhi ya wakazi Zimmerman wanalalamikia kukithiri kwa visa vya wizi. “Eneo la Canopy na Base, kufikia saa mbili za jioni watu huibwa hadharani na kundi la wahuni wanaoendelea kutuhangaisha,” alisema mama mmoja.

Wenyeji walisema licha ya asasi za usalama kufahamishwa kukita mizizi kwa visa vya wizi, hakuna hatua yoyote imechukuliwa kufikia sasa. “Kila siku jioni huwa tunatazama gari la askari likipiga doria kukusanya pesa kwa mabaa na vituo vya kuuza pombe, lakini wakati wa kuimarisha usalama hawana,” walishangaa wakazi.

Mtaa wa Zimmerman ni karibu kilomita mbili kutoka kituo cha polisi cha Kasarani.

You can share this post!

Vijana wapatao 30 wazindua biashara ya kuchonga viazi Thika

CBK yashikilia tafsiri sahihi ya ‘Bank’ ni...

adminleo