• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 2:25 PM
Mahakama yasimuliwa jinsi mauaji ya wanafunzi 145 yalitekelezwa

Mahakama yasimuliwa jinsi mauaji ya wanafunzi 145 yalitekelezwa

Na RICHARD MUNGUTI

MSONGO wa mawazo na hisia mseto kuhusu mauaji ya kinyama ya wanafunzi 145 wa chuo kikuu cha Garissa yaliwakumba wazazi waliofika kortini Jumatano kufuata uamuzi wa kesi ya mauaji ya watoto wao 145 katika chuo kikuu cha Garisa yapata miaka minne iliyopita.

Huku hakimu mkuu wa mahakama ya Milimani Francis Andayi akikariri ushahidi ulivyotolewa na mashahidi 22 kimya kingi kilitanda ukumbi wa mahakama huku kamera za video zikimumulika akiendelea kukariri ushahidi ulivyosemwa.

Hatimaye Andayi aliwapata na hatia washukiwa watatu kati ya watano, ndipo waliokuwa mahakamani walipumua na kuwatazama washtakiwa hao korti iliposema, “Nyinyi ni magaidi wa Al Shabaab walioshambulia chuo kushurutisha Kenya kuondoa maafisa wake wa kijeshi nchini Somalia. Mlishirikiana na magaidi wanne kuwaua wanafunzi wasio na hatia ambao ndoto, ari na shauku ya kusoma mliikatiza pasi na sababu. Wanafunzi hawa hawakuwakosea chochote.”

Hata hivyo kati ya mashtaka 156 dhidi ya washtakiwa Andayi alifutilia mbali mashtaka mawili dhidi ya ‘gaidi’ mmoja Rashid Mberesero aliyesema hajulikani ikiwa ni “Mkenya au Mtanzania.”

Andayi alikariri jinsi magaidi wanne waliokuwa wamejihami kwa bunduki aina ya Ak 47 walivamia chuo hicho mwendo was aa kumi na asubuhi na kuanza kuwaua wanafunzi kiholela.

“Wanafunzi waliokuwa wamekesha katika maombi waliuawa kinyama na kurundikwa katika chumba cha maombi,” alisema Andayi.

Magaidi walikuwa wakiita majina ya viongozi wa wanawafunzi wawaangamize, alikumbuka hakimu.

“Piga risasi ya miguu wote wanaojaribu kuvuka ua la seng’enge,” mmoja wa magaidi alimwamuru mwenzake.

Wanafunzi wengi waliojaribu kutoroka walivunjwa miguu huku sita wakiuawa wakijaribu kutoroka.

Ijapokuwa Mberesero aliachiliwa kwa mashtaka mawili ya kupatikana nchini kinyume cha sheria akiwa raia wa Tanzania, hakimu alimpata na hatia ya kuwa mwanachama wa kundi la kigaidi la Alshabaab.

Ushahidi uliowasilishwa ulisema kuwa washtakiwa hao pamoja na magaidi wanne waliokuwa wamevalia magwanda ya kijeshi “walikuwa wanawakusanya wasichana na kuwadanganya wanawaepusha balaa ila kuwageuka na kuwalaza chini kwa foleni na kuwapiga risasi mmoja baada ya mwingine huku wakiwaambia wao ni Al Shabaab na lazima Serikali ya Kenya iwaondoe maafisa wake wa jeshi Somalia.”

Akimwachilia Rashid Mberesero, hakimu mkuu Francis Andayi, aliwalaumu maafisa wa usalama, kutowasilisha ushahidi kubaini uraia wa mshtakiwa.

Alisema shtaka hilo la kupatikana na akiwa nchini bila kibali rasmi cha ugeni ama kitambulisho cha Kenya halikuthibishwa na kiongozi wa mashtaka Duncan Ondimu.

“Kwa vile hakuna ushahidi kuthibitisha Mberesero ni raia wa Tanzania, sina budi ila kuitupilia mbali na kumwachilia huru. Sijui ikiwa ni Mkenya ama Mtanzania.”

Punde tu shtaka hilo lilipotupiliwa mbali mshtakiwa alisimama kizimbani na kusema “Asante mheshimiwa. Nashukuru niko huru.”

Hatimaye aliposikia atarudishwa gereza kuu la Kamiti alizusha na kumwuliza hakimu “uliniwachilia awali naenda kufanya nini Kamiti.”

Lakini Andayi kwa upole akamweleza Mberesero aliachiliwa kwa kosa la kupatikana nchini bila idhini akiwa raia wa Tanzania lakini shtaka la mauaji bado linamkabili.

You can share this post!

Mutyambai azima polisi waliozoea hongo katika vizuizi...

Alai ndani siku 14 kwa ‘kufurahia Al Shabaab wakiua...

adminleo