• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 6:55 AM
Makundi ya kupigia debe DP Ruto eneo la Mlima Kenya yasema hayatasitisha harakati

Makundi ya kupigia debe DP Ruto eneo la Mlima Kenya yasema hayatasitisha harakati

Na MWANGI MUIRURI

MAKUNDI kadhaa yanayompigia debe Naibu Rais William Ruto kurithi urais katika uchaguzi mkuu wa 2022 yamemtaka Rais Uhuru Kenyatta ajifahamishe na uhalisia kwamba harakati zao hazitazimika kwa vyovyote vile.

Makundi hayo yakijifahamisha kama Hustler Nation, Ruto@10 Fresh na Sasa ya Ruto10 – yote yakiwa ndani ya uratibu wa Timu Tangatanga – yalisema Jumatano kuwa “Rais apende asipende lazima tuendeleze ajenda ya Ruto hadi 2032.”

Samuel Maina msemaji wa kuratibu vuguvugu zilzo ndani ya timu hiyo ya kisiasa, alisema, “Rais ndiye alitupa msingi wa kufuata Ruto na kutangatanga naye hadi 2032.”

Alisema kuwa kwa sasa ni unafiki mkuu kutoka kwa Rais kuzima siasa kuchezwa za urithi “ikizingatiwa kuwa wewe ndiye ulitupa mbinu ya kuzurura kote nchini kushiriki maombi na harambee makanisani ukisaka mbinu ya kujinasua kutoka kesi yako ya Hague na pia kushinda uchaguzi wa 2013 na ule wa 2017.”

Bw Maina pia alimtaka rais aelewe kuwa “mwaka wa 2013 tulisimama na wewe kama jamii za Mlima Kenya tukijua tulikuwa tunakupa makali ya kujinasua Hague kupitia kukupa mamlaka ya rais Ikulu.”

Katika hali hiyo, Bw Maina alimtaka rais aelewe kuwa ni dharau kuu kusimama hadharani leo hii kudai kuwa yeye ndiye alisaidia wengine kupata mamlaka.

“Unataka kusema kuwa ungekosa kuwania urais leo hii hatungekuwa na wabunge, maseneta, wawakilishi wa wanawake, madiwani na magavana?” akahoji Bw Maina.

Alisema kuwa Rais Kenyatta ndiye aliambia Mlima Kenya kuwa “mimi nitatawala miaka 10 na Ruto atawale miaka 10.”

Kikao cha hadhara

Alimtaka Rais Kenyatta aandae kikao cha hadhara jinsi alivyokuwa akiahidi Ruto urithi hadharani na atangaze kuwa amebadiliasha mawazo.

“Unatukemea kwa nini tukipigia Ruto debe ilihali wewe ndiye ulituchochea kufanya hivyo? Mbona utuambie kuwa tunarandaranda mashinani ilihali wandani wako wapya wa handisheki na Kieleweke wanazunguka kila mahali wakitushambulia? Unataka kugeuza Naibu wako wa Rais kuwa vibonde bila kufahamu akipigwa ni serikali yako inapigwa?” akahoji.

Bw Maina alitangaza kuwa harakati zote za Tangatanga zitaendelea mbele bila kuzingatia hasira, dharau, matusi na vitisho vya Rais.

You can share this post!

Baraza la Agikuyu sasa lamtaka Rais atangaze msimamo wake...

Matokeo ya DNA yamwokoa mwalimu aliyedaiwa kupachika mimba...

adminleo