• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Matokeo ya DNA yamwokoa mwalimu aliyedaiwa kupachika mimba mwanafunzi

Matokeo ya DNA yamwokoa mwalimu aliyedaiwa kupachika mimba mwanafunzi

NA PHYLLIS MUSASIA

MWALIMU mmoja wa shule ya upili ambaye alisimamishwa kazi kufuatia madai kuwa alimpachika mimba msichana wa kidato cha tatu 2018, amefika mahakamani baada ya uchunguzi wa chembechembe za DNA kuonyesha kuwa yeye si baba wa mtoto wa msichana huyo.

Bw Philip Lang’at ambaye alikuwa mwalimu katika Shule ya Upili ya Mawingu eneobunge la Kuresoi Kaskazini, alishutumiwa kwa madai ya kuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi na mwanafunzi wa shule hiyo.

Hata hivyo, matokeo ya DNA yaliofanywa na maabara ya serikali ya Kisumu yalionyesha kuwa, Bw Lang’at hana uhusiano wowote wa damu na mtoto huyo.

Mnamo Januari 19 mwaka huu, Bw Lang’at alirekodi malalamishi yake katika kituo cha polisi cha Kuresoi na kushikilia kwamba hakuwa na uhusiano wowote na mwanafunzi na kwamba alikuwa anahangaika kimawazo kufuatia shutuma hizo za uongo.

Wakati huo, mwalimu huyo alikuwa anakumbana na mashtaka ya unajisi pamoja na kushiriki tendo la ndoa na msichana mwenye umri mdogo.

Hii ni kulingana na ripoti iliotolewa na idara ya uchunguzi wa maswala ya jinai ya Kuresoi kufuatia malalamishi hayo yaliorekodiwa kwenye stakabadhi nambari 2/201. Ilitokana na amri ya kamati ya urekebishaji tabia ya Tume ya Kuwaajiri Walimu nchini (TSC) iliyoandaa kikao mnamo Oktoba 12, 2018.

Kwenye ripoti hiyo iliyoonekana na Taifa Leo Dijitali, TSC ilihoji kuwa mwalimu huyo alikosa maadili kama ilivyo kwenye sheria ya tume hiyo jambo lililompelekea kupokezwa barua ya kusimamishwa kazi na baadaye kutupwa nje.

Bw Philip Lang’at aliyesimamishwa kazi kufuatia shutuma za kumtia mimba mwanafunzi. Matokeo ya vipimo vya DNA yamemwondolea aibu na lawama. Picha/ Phylis Musasia

Hata hivyo, kulikuwepo na madai kuwa mwalimu Lang’at alikuwa akiwasiliana na mwanafunzi huyo kupitia njia ya simu na hata kumtumia pesa kupitia M-Pesa jambo ambalo shirika la mawasiliano la Safaricom lilikosa kuthibitisha.

Hata hivyo, kuonana kwa wawili hao wakiwa shuleni kama mwalimu na mwanafunzi ndio huenda ingebakia kuwa ithibati kwamba wawili hao walikuwa kwenye uhusiano.

Kwenye barua ya Mei 16, 2018 iliyoandikwa na bodi ya usimamaizi wa shule hiyo, mwalimu huyo alitakiwa kuandika barua iliyoelezea ni kwa sababu gani hakuchukuliwa hatua za kisheria.

“Ni ni kukujulisha ya kwamba umehusishwa na madai ya kumpachika mimba mmoja wa wanafunzi wa kike kwenye shule hii na hivyo basi unazo siku 14 kuandika sababu za kukuzuia kukosa kuchuliwa hatua za kisheria,” ikasoma barua hiyo.

Kulingana na ripoti ya idara ya uchunguzi wa jinai iliyofuatilia kesi hiyo kwa karibu, mwalimu Langa’t alisemekana kuwa na uhusiano mbaya wa kikazi na mwalimu mkuu wa shule ya Mawingu Bw Wilson Salpei

“Bw Salpei ambaye alisemekana kumtongoza mwalimu mmoja wa kike aliyekuwa ameajiriwa kazi na bodi ya shule hiyo, hakuweza kufaulu kwenye juhudi zake za kumleta karibu mwalimu huyo ambaye baadaye alionekana kuwa na urafiki wa karibu sana na Bw Lang’at. Kutokana na jambo hilo, uhasama ulizuka baina ya wawili hao na kupekelea sarakasi hizi,” ikasoma ripoti hiyo iliyondaliwa na afisa mpelelezi Bw Alexander Mutie.

Ripoti hiyo hata hivyo ilipelekea idara hiyo kuagiza kukamatwa kwa Bw Salpei pamoja na wote waliotoa ushahidi wa uongo kwa tume ya TSC pamoja na polisi.

Salpei alishtakiwa Jumatatu pamoja na Bi Jane Rono ambaye ni mwenyekiti wa bodi ya shule hiyo, mwanafunzi mwathiriwa pamoja na mamaye.

Wane hao walifikishwa mbele ya hakimu wa korti ya Molo Bi Alice Mukenga ambapo walikabiliwa mashtaka ya kuungana na kutoa habari za uongo dhidi ya Bw Lang’at.

Aidha, Bw Salpei pamoja na Bi Rono walishtakiwa pia kwa kutumia mamlaka yao vibaya na kumshtumu mwalimu. Mwalimu huyo mkuu pia alitakiwa kujibu mashtaka ya kumdhulumu mwalimu wa kike kimapenzi na kisha kumfuta kazi.

 

You can share this post!

Makundi ya kupigia debe DP Ruto eneo la Mlima Kenya yasema...

AFCON: Timu zitaumiza nyasi katika viwanja hivi

adminleo