• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 11:14 AM
Bwana Harusi sasa aahirisha fungate baada ya sherehe kugeuka msiba

Bwana Harusi sasa aahirisha fungate baada ya sherehe kugeuka msiba

Na MOHAMED AHMED

BWANAHARUSI katika sherehe ya harusi iliogeuka kuwa msiba kwa familia za watu sita eneo la Mishomoroni, Mombasa Jumatatu alieleza kuwa alilazimika kusitisha kuenda fungate baada ya mkasa huo.

Sadam Ziro mwenye umri wa miaka 34 ameshindwa kupata usingizi baada ya siku hiyo aliyoitarajia kuwa ya furaha tele kugeuka kuwa msiba.

Akizungumza na Taifa Leo katika mtaa wa Tua Tugawe nyumbani hapo kulipotokea mkasa huo Bw Ziro aliutaja mkasa huo kama “nuksi” ambayo imemuepuka.

“Nashukuru Mungu hakuna aliyedhurika kati yangu na mke wangu. Kuporomoka kwa shimo hilo lilikuwa sababu tu ya kuepuka kitu kibaya zaidi lakini nahisi uchungu kwani siku yangu ya furaha ndiyo imekuwa sababu ya kufa kwa watu hususan watoto,” akasema Bw Ziro.

Bw Ziro ambaye ni fundi wa mifereji alisema kuwa mipango yake ya kumpeleka mke wake Fatma Jumaa, 25 kwa fungate eneo la Ukunda Kaunti ya Kwale imeingia doa.

“Nilikuwa nimepanga mengi kama mwanamume yeyote yule ambaye angempangia mkewe ili kumfurahisha lakini siwezi kukosoa mipango ya Mungu,” akasema Bw Ziro.

 

Lawama

Alizungumza wakati familia za waliofariki zikiendelea kuomboleza wapendwa wao na huku zikiilaumu serikali ya kaunti kwa kutotekeleza wajibu wake katika ukaguzi wa mashimo suala ambalo walisema lilisababisha vifo vya wapendwa wao.

Huku familia hizo zikiendelea kupambana na hali ya masikitiko pia walimlaumu mmiliki wa nyumba ambapo kulikoandaliwa harusi kwa kutotekeleza wajibu upande wake.

Jamaa hao waliongea kwa uchungu wa kupoteza wapendwa wao waliofariki katika mkasa huo ambao wengi walikuwa watoto wadogo.

“Hatuwezi kulaumu mipango ya Mungu lakini kuna mambo ambayo kama binadamu tunaweza kuepuka iwapo tutafanya mambo ipaswavyo. Kabla ya tukio la juzi tayari kulikuwa na matukio mengine yaliohusisha mashimo hayo na serikali ya kaunti ikasema itafanya ukaguzi wa mashimo hayo lakini kwa sababu ya uzembe ndio tumeweza kupoteza wapendwa wetu,” akasema Bw Amir Salim ambaye ni jama ya familia iliopoteza watoto wawili.

Familia hiyo ya Bw Masoud Mwalim ilipoteza watoto wawili Mohamed Mwalim wa miaka saba na Masoud Mwalim mwenye miaka 14.

Wawili hao walikuwa miongoni mwa sita waliotumbukia ndani ya shimo la choo la zaidi ya futi 50 walipokuwa wamehudhuria harusi hiyo.

 

Wanafunzi

Wengine walioaga ni pamoja na Munira Adam ambaye ni mwanafunzi wa darasa la sita na Habiba Mohammed wa darasa la nane. Fatma Feiswal, mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya upili ya Mtopanga na mwanamke wa miaka 35.

Abdallah Feiswal ambaye ni nduguye Fatma mwenye umri wa miaka 20 vile vile aliulaumu usimamizi wa serikali kwa kutotekeleza ahadi ya kukagua mashimo hayo.

“Nimepoteza dadangu kwa sababu ya makosa ya watu wengine. Hatuwezi kulaumu waliofariki kwa kuhudhuria harusi lakini ni wazi kuwa iwapo mashimo hayo yangekuwa yamekaguliwa basi tusingepatikana na mkasa huo,” akasema Bw Feiswal.

Mnamo Jumapili mkurugenzi wa askari wa kaunti Mohammed Amir alisema kuwa kitengo hicho kitaanzisha ukaguzi wa mashimo ya choo ambayo hajayafinikwa vizuri ili kuepeka maafa zaidi.

 

Alama ya ilani

“Tutahakikisha kuwa mashimo hayo yanafunikwa na simiti yakiwa yamewekwa vyuma na sio mbao au mabamba tu. Vile vile tutazunguka kuhakikisha kuwa mashimo hayo yamewekwa alama ya kuonya watu wasisimame juu yake,” akasema Bw Amir.

Hata hivyo, pita pita ya Taifa Leo katika eneo hilo la mkasa iligundua kuwa ukaguzi huo haujaanzishwa.

Baadhi ya mashimo hayo ambayo yalikuwa hayajafinikwa vizuri bado yalikuwa yamesalia katika hali ile ile.

Mzee wa mtaa huo Joseph Deng’ea alisema kuwa licha ya kujitolea kuanza kuyatambua baadhi ya mashimo hayo maafisa wa kaunti hawakujitokeza kwa ajili ya zoezi hilo.

“Tusingetaka kuona maafa zaidi kwa sababu ya mashimo haya. Sisi tumejitolea kufanya kazi pamoja na kaunti lakini wametuangusha. Ni lazima usimamizi wa kaunti uhakikishe kuwa mashimo haya yamefinikwa ipaswavyo kama walivyoahidi,”  akasema.

 

You can share this post!

Wezi waliopiga kambi nyumbani kwa bwenyenye kwa wiki moja...

Uhuru aagiza polisi waliohudumu kwenye Uchaguzi Mkuu...

adminleo