• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 10:55 AM
Kanisa Katoliki lawarai Wakenya kufaana maishani

Kanisa Katoliki lawarai Wakenya kufaana maishani

NA RICHARD MAOSI

DAYOSISI ya Kanisa Katoliki Nakuru Jumapili iliandaa misa maalum katika shule ya wasichana ya Nakuru, kuadhimisha siku ya bendera ya Amerika. 

Muungano wa wanafunzi Young Catholic Student Association (YCSA) uliandaa sherehe hiyo inayoratibiwa kila mwaka ili kutoa shukrani.

Vijana kati ya miaka 14-35 wamekuwa wakishiriki katika hafla hii inayotoa hamasisho kuhusu utunzaji wa mazingira na kuwasaidia wasiojiweza katika jamii.

Shughuli yenyewe iliwaleta pamoja wanafunzi zaidi ya 2500 kutoka shule 50 katika kaunti za Nakuru, Baringo na Elgeyo Marakwet.

Waliohudhuria ni pamoja na askofu Wycliffe Karathi, John Ngige na Francis Muraya kutoka dayosisi ya Nakuru.

Askofu Karathi aliwaomba wanafunzi kutumia maarifa wanayopata shuleni ili kujiendeleza kwa ajili ya manufaa yao siku za usoni.

Aliwaeleza kuchangia katika sekta ya ubunifu kwa kutoa mawazo yatakayoifaa jamii na uwekezaji, ikizingatiwa kuwa wao ndio viongozi wa kesho.

“Kanisa limejitolea kwa hali na mali kuhakikisha vijana wanajiunga na makundi ya kidini ili kuleta wimbi la mabadiliko katika ulimwengu wa sasa, unawapa vijana changamoto nyingi,” akasema.

Akizungumza na Taifa Leo Dijitali, mwakilishi wa vijana katika dayosisi ya Nakuru, aliongezea kuwa muungano wa YCSA unajumuisha vijana ambao ni wacha Mungu.

Alisema kuwa ni fahari yake kubaini kua, japo shule nyingi nchini Kenya haziendeshwi na kanisa katoliki bado kuna vijana wengi wanaoshikilia imani ya kikatoliki.

Aliongezea kuwa wanafunzi wamekuwa wakijichangia pesa kwa makundi ili kufanikisha miradi inayowaleta pamoja kwenye kumbi mbalimbali ndani na nje ya kaunti ya Nakuru.

“Kinachowapatia motisha ni wito kutoka kwa Baba Mtakatifu wawe watu wa kujali maslahi ya kijamii na wachangie katika utunzaji wa mazingira,” alisema.

Aidha wanafunzi walipata fursa ya kuonyesha vipaji vyao kwenye jukwaa kwa kuimba nyimbo na kukariri mashairi.

Ann Nyawira mwanafunzi wa kidato cha pili kutoka shule ya wasichana ya Bahati, hakuficha furaha yake alipozungumza na wanahabari.

Alisema hii ni mara yake ya kwanza kuhudhuria tamasha kama hii ambayo imemsaidia kupata jukwaa la kubadilishana mawazo na wanafunzi wenzake.

Anasema amejifundisha kuwa na moyo wa kugawa kile kidogo alicho nacho kwa maskini wasiokuwa na njia ya mapato.

Siku yenyewe inafaa kuwaombea wanaokinzana na unyanyasaji, kutokana na ukosefu wa haki,vita na majanga ya kitaifa.

Kulingana na ujumbe wa baba mtakatifu maadhimisho haya yanastahili kuambatanishwa na vitendo bali sio maneno tu.

You can share this post!

Wawika nje, baridi bungeni

Wabunge vijana wanavyozembea mijadala muhimu bungeni

adminleo