• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 3:04 PM
Watakaozima michango makanisani wataangamizwa na Mungu – Ruto

Watakaozima michango makanisani wataangamizwa na Mungu – Ruto

DERICK LUVEGA na CHARLES WASONGA

NAIBU Rais William Ruto amewasuta wanasiasa wanaopanga kudhibiti michango kanisani kupitia mswada bungeni, akisema wataangamizwa na hasira za Mungu.

Akiongea Jumapili katika kaunti ya Vihiga wakati wa sherehe ya kuadhinisha miaka 70 tangu kuanzishwa kwa Kanisa la African Divine (ADC) nchini, Dkt Ruto aliwataka wabunge kuukataa mswada huo wa kudhibiti michango ya zaidi ya Sh100,000.

Alikuwa akimlenga kiongozi wa wachache katika bunge la kitaifa John Mbadi ambaye amedhamini mswada wa marekebisho ya Sheria kuhusu Uongozi na Maadili ya watumishi wa umma kwa lengo la kupambana na ufisadi.

Inasemekana kuwa Bw Mbadi ambaye ni Mbunge wa Suba Kusini aliwasilisha mswada huo kutokana na ushauri wa kiongozi wa ODM Raila Odinga ambaye amekuwa akipinga mienendo ya wanasiasa kutoa pesa nyingi kama michango kanisani.

Dkt Ruto akasema: “Watu wanataka kutumia bunge kuyumbisha kazi ya Mungu. Hizi ni ishara ya siku za mwisho. Nataka kuwaambia wabunge kwamba wakipitisha mswada unaohujumu kazi ya Mungu…. Wajue kwamba wataangamia.”

Naibu Rais alisema kwua makanisa mengi ambayo yalibuniwa na Waafrika yanakabiliwa na changamoto nyinyi kwa sababu hayana ufadhili kutoka ng’ambo, kwa hivyo yanastahili kusaidiwa.

Dkt Ruto aliwashauri wabunge kuwasilisha miswada ambayo inaweza kuimarisha sekta za Elimu, Maji, Miundo Msinga , Afya na miongoni mwa zingine badala ya kudhamini miswada inayohujumu kazi ya Mungu.

Naibu Rais alitangaza kuwa ametoa Sh3 milioni kama mtaji wa kuanzishwa kwa Chama cha Akiba na Mkopo cha Kanisa la ADC kinacholenga kuwasaidia zaidi ya mapasta 4,000 wa kanisa hilo.

Vile vile, Dkt Ruto alisema kuwa ameweka jiwe la msingi kwa mradi wa ujenzi wa Ukumbi mkubwa wa ibada katika makao makuu ya ADC eneo la Boyani.

Askofu Mkuu wa Kanisa hilo John Chabuga pia aliwakaripia wanasiasa wanaopinga michango kanisa akisema watalaaniwa na Mungu.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na wanasiasa kadha kutoka uliokuwa mkoa wa magharibi kama vile wabunge’ Benjamini Washiali (Mumias Mashariki), Malulu Injendi (Malava), Charles Gimose (Hamisi). Wengine walikuwa Gavana wa Vihiga Wilbur Otichillo, aliyekuwa Gavana Moses Akaranga na aliyekuwa Seneta wa Kakamega Boni Khalwale.

Viongozi hao waliunga mkono azma ya Dkt Ruto kuwania urais 2022 wakitoa wito kwa jamii ya Waluhya kumuunga mkono ili wawe serikalini.

 

You can share this post!

Vunjeni ‘Tangatanga’ na...

Sasa nataka ubingwa wa EPL, Klopp asema

adminleo