Habari Mseto

Makahaba 800 walia kuteswa na polisi, wataka waheshimiwe

June 25th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na PHYLLIS MUSASIA

MAKAHABA zaidi ya 800 mjini Nakuru wamelalamikia kuteswa na kudhulumiwa na maafisa wa kaunti pamoja na polisi.

Hii ni baada ya Kamishna wa Kaunti, Bw Erustus Mbui kutishia wiki iliyopita kuwaondoa makahaba hao kutoka mjini kufuatia ongezeko la idadi yao ambayo sasa imezua utata wa kiusalama.

Akizugumza na Taifa Leo, mwenyekiti wa makahaba hao, Bi Daisy Achieng chini ya chama cha ‘Smart Ladies,’ aliwataka maafisa hao kuwa na utu na kuheshimu kazi wanayoifanya na wala si kuwaona kama watu wasiokuwa na umuhimu katika jamii.

Bi Achieng alilalamikia kukamatwa kwa wanachama kiholela na maafisa wa polisi ambao alidai kuwa wanatumia mbinu mbovu ambayo huwaumiza makahaba na kuwaacha wakiuguza majeraha mabaya.

“Polisi pamoja na maafisa wa kaunti hawana heshima kwetu sisi. Jinsi wanavyofika hapa na kututia pingu haifai kabisa. Wengine wao wanatumia nguvu kupita kiasi na kukamata akina dada hawa kwa njia isiyokubalika,” akalalamika Bi Achieng.

Alisema maafisa hao wanapaswa kutoa usalama wa kutosha kwa raia wa tabaka zote na wala sio kuwadhulumu watu ambao wako kazini kutafuta riziki ya kila siku kwa ajili ya maslahi ya familia zao.

“Tuko takribani makahaba 800 ambao tunafanya kazi kwenye mji huu. Na wakati wote sisi hulipa ushuru kutokana na kazi hii, kwa hivyo maafisa wa polisi wajiepushe na jinsi wanavyotukamata kiholela haswa tukiwa kazini,” akaeleza Bi Achieng.

Wikendi iliyopita, Bi Achieng alisema kuwa takribani makahaba 100 walitiwa mbaroni na kufikishwa kortini Jumatatu, ambapo walishtakiwa kwa kuzurura mjini bila sababu na kusababisha usumbufu.

“Wale waliofikishwa mahakamani walitozwa faini ya Sh 3, 000 kila mmoja faini ambayo wengi wao walishindwa kulipa na kuomba msaada kwani siku hiyo hawakuwa wamepata hela zozote walipokamatwa,” akaongeza Bi Achieng.

Mkuu wa polisi wa kata ndogo ya mji wa Nakuru Mashariki, Bi Ellena Wanjiru alikiri kuhusu msako lakini akasema haukulenga kundi lolote. Aliwataka wenye madai ya dhuluma, wayawasilishe kwao.