Habari Mseto

KCB yasema kiwango cha riba kimeipunguzia mapato

March 14th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na BERNARDINE MUTANU

Benki ya KCB imetangaza faida ya Sh19.7 bilioni mwaka wa 2017 baada ya kutozwa ushuru.

Faida hiyo haikupanda, suala ambalo benki hiyo ilisingizia kudhibitiwa kwa viwango vya riba na Benki Kuu.

Hii ni kulingana na benki hiyo Alhamisi, wakati wa mkutano wa washikadau.

Mapato yake kutokana na mikopo yalishuka kwa Sh39 milioni, licha ya mikopo kuongezeka kwa asilimia 10. Jumla ya mikopo iliyotolewa na benki hiyo katika kipindi hicho ilikuwa Sh422.7 bilioni.

Hata hivyo, idadi ua wateja walioweka pesa iliongezeka kwa asilimia 11.5 ambapo jumla ya Sh449.6 milioni iliwekwa humo.

Benki hiyo ilithibiti viwango vya riba kwa pesa zilizowekwa kwa lengo la kupunguza hasara zaidi.