• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 12:26 PM
Spika Muturi aagiza wanahabari wapewe viti bungeni

Spika Muturi aagiza wanahabari wapewe viti bungeni

Na CHARLES WASONGA

SPIKA wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi Alhamisi amewaamuru wenyekiti na makarani wa kamati za bunge wahakikishe kuwa wanahabari wanaoalikwa kuripoti shughuli za kamati hizo wanapewa viti na mazingira faafu ya kukusanya habari.

Akiongea bungeni, Bw Muturi alisema ni aibu kwa wanahabari kuketi sakafuni ilhali wao hutekeleza wajibu mkubwa wa katika kufahamisha umma kuhusu mambo yanayoendelea bungeni.

“Wanahabari ni washirika wakuu wa asasi hii. Wao ndio huunganisha bunge na umma kwa kuwafahamisha yanayojiri katika ukumbi huu na kamati mbalimbali. Kwa hivyo, watu hawa hawafai kushushwa hadhi kwa kulazimishwa kuketi chini jinsi picha kadhaa zinazozunguka mitandaoni zinaonyesha,” akasema.

Bw Muturi alisema hayo kufuatia kisa ambacho wanahabari walioalikwa kuripoti matukio katika Kamati ya Bunge kuhusu Haki na Masuala ya Kikatiba (JLAC) kulazimika kuketi sakafuni kwa kukosa viti.

Baadhi yao walinasa picha za wenzao wakiketi sakafuni na kuzisambaza katika mitandao ya kijamii kama vile Twitter, Facebook na WhatsApp. Aidha, walisambaza picha hizo kwa Bw Muturi, Kiongozi wa wengi Aden Duale na Baraza la Vyombo vya Habari (MCK).

Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Baringo Kaskazini William Cheptumo ilikuwa inapokea ripoti kutoka na maafisa wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) wakiongozwa na mwenyekiti Askofu mstaafu Eliud Wabukala kuchambua ripoti kuhusu kesi za ufisadi tangu 2014 hadi mwaka huu.

Kulingana na wanahabari hawa, hali hii si geni. Imekuwepo tangu Kenya ipate uhuru. Picha/ Charles Wasonga

Lakini, kulingana na wanahabari hao, hali kama hiyo sio geni.

“Hali hii hutokea katika takriban kamati zote. Kuna viti vichache ambavyo havitoshi wabunge, mashahidi na wanahabari. Hii ndio maana baadhi yetu huishia kuketi sakafuni,” mwanahabari mmoja ambaye aliomba jina lake libanwe aliambia Taifa Leo Diijitali.

Vifaa muhimu havipo

Hata hivyo, madhila yao huwa hayaishi hapo. Kando na kuketi sakafuni au kusimamia kwa saa nyingi wakifuatialia habari kama vikao vya kamati, vyumba hivyo vya mikutano kwa kawaida havina vifaa vya sauti au mwangaza faafu.

“Hali kama hii hupelekea wapiga picha kutonasa picha na sauti nzuri,” ripota mwingine wa kituo cha runinga ya KTN akasema.

Wanahabari hao wanasema kuwa wenyekiti wa kamati huendesha shughuli zao pasi na kujali changamoto wanazokumbana nazo.

“Lakini wao huwa wepesi kulalamika wakati habari kuhusu shughuli za kamati zao hazijaangaziwa katika vyombo vya habari,” anaongeza mwanahabari huyo ambaye ameripoti masuala ya bungeni kwa zaidi ya miaka 10.

Wanahabari hao wanasema kuwa wamekuwa wakiwasilisha malalamishi yao kwa maafisa washirikishi wa kitengo cha habari lakini hamna hatua zozote zimechukuliwa.

You can share this post!

Mwangi Kiunjuri asema madai ya uhai wa Ruto kuwa hatarini...

Nanok aadhibiwa na ODM kwa kujiunga na Tangatanga

adminleo