Habari

Mzaha wa kupeleka mizigo Nairobi na kuirejesha Mombasa

June 28th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na ANTHONY KITIMO

WAFANYABIASHARA jijini Mombasa wanaoagiza bidhaa kutoka ng’ambo, wamelalamikia hatua ya serikali kuwaagiza kusafirisha mizigo yao hadi Nairobi kukaguliwa na kulipia ushuru na kisha kuisafirisha tena hadi Mombasa.

Wafanyibishara hao wanasema hatua hiyo itaongeza gharama ya kufanya biashara.

Wamesema hawaelewi sababu za kupeleka shehena zao hadi kituo cha Inland Container Depot jijini Nairobi kwa reli ya kisasa (SGR) licha ya mizigo hiyo kuandikishwa kuwa ni ya Mombasa.

Bw Michael Kabuga, mmoja wa wafanyibishara hao, alisema amelazimika kulipa zaidi ya Sh109,446 za kuhifadhi shehena yake Nairobi, ada ya SGR na gharama ya kurudisha mizigo yake hadi Mombasa.

“Stakabadhi zote za kuagiza shehena zangu zimesajiliwa mjini Mombasa na kuzipeleka Nairobi ni jambo litakalosababisha kuchelewesha kufika kwa mizigo hiyo na pia kuongeza gharama,” akasema Bw Kabuga.

Wafanyibiashara hao wanalazimika kulipia Sh85,000 kwa reli ili mizigo yao kusafirishwa tena hadi Mombasa.

Stakabadhi zilizodhihirisha shehena hizo kupelekwa Nairobi zinaonyesha kuwa wafanyibiashara hao watalazimika kulipia kati ya Sh70,000 na Sh120,000 kama ada inayotozwa mizigo kuhifadhiwa zaidi ya siku nne eneo la ICD.

Mwaka uliopita, Shirika la Reli nchini lilitangaza kuwa mizigo yote itakayoagizwa kutoka ng’ambo itasafirishwa kwa SGR hadi Nairobi ili kuongeza mapato ya shirika hilo linalodaiwa zaidi ya Sh327 bilioni na serikali ya China kwa kujenga SGR.

Kwa muda wa wiki moja iliyopita, bandari ya Mombasa iliripoti kupunguza msongamano mkubwa katika bandari hiyo baada ya kuanzisha mkakati maalumu wa kupakia mizigo moja kwa moja kutoka kwa meli hadi kwa reli.

Zaidi ya shehena 1200 husafirishwa kila siku kwa reli baada ya shirika la reli kuongeza mabogi ya mizigo hadi 12 katika kipindi cha miezi miwili iliyopita.

Tangu SGR kuanza kupeleka mizigo moja kwa moja hadi Nairobi, kampuni za kuhifadhi mizigo (CFS) zimepungua na kulazimika kuhamia eneo la Embakasi, Nairobi huku wengine wakijitayarisha kuwekeza eneo la Naivasha.

Kutokana na kuongezeka kwa idadi ya mizigo inayosafirishwa hadi ICD Nairobi, serikali imeanza upanuzi wa sehemu ya kupokea shehena eneo hilo ili kuhifadhi zaidi ya shehena 450,000.