Makala

NGILA: Ushirikiano kueneza elimu ya dijitali nchini upigwe jeki

June 28th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA FAUSTINE NGILA

USHIRIKIANO baina ya Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Watoto (UNICEF), kampuni ya teknolojia ya Nokia na Wizara ya Elimu ya Kenya uliotangazwa majuzi kueneza elimu ya dijitali miongoni mwa wanafunzi Wakeny, unafaa kupongezwa.

Ingawa mpango huo bado ungali katika hatua za mwanzo, watoto wa shule za msingi nchini hatimaye wataweza kufundishwa kuhusu masuala ibuka ya kiteknolojia, bila kuwatenga walio katika shule za mashinani.

Kilichotia moyo kuhusu ushirikiano huu ni kuwa mashirika hayo yalitambua ukosefu wa elimu ya teknolojia nchini, licha ya serikali ya Jubilee kuahidi kila mwanafunzi wa Darasa la Kwanza kipakatalishi.

Ni aibu iliyoje kwa serikali iliyojinadi kwa wapigakura jinsi ingeeneza vifaa vya kidijitali hadi vijijini, kulemewa kutimiza ahadi kama hii huku fedha zikiibwa katika mashirika kadha ya serikali bila kujali adhabu.

Nina imani ahadi hiyo ilitolewa kuvutia wapigakura na wala si kwa haja ya kukuza kizazi cha siku za usoni kujenga uchumi wa taifa hili kwa kutumia teknolojia.

Na sasa miaka kadha baadaye, mashirika tajika yameungana kufufua wazo hilo kupitia kwa Taasisi ya Ukuzaji Mtalaa nchini (KICD), ambapo mpango mzima ni kuhakikisha intaneti imeenezwa hadi mashinani.

Kwa kuwa serikali ilishindwa kuetekeleza ahadi yake, sasa inafaa kupiga jeki mpango huu kwa kuhakikishia washirika mazingira yafaayo kunoa akili za watoto wetu kwa uchumi wa miaka ya usoni.

Washikadau wote katika elimu na teknolojia wanafaa kuvalia njuga mradi huu. Ushirikiano dhabiti unahitajika baina ya walimu, wazazi, wanafunzi, kampuni za mawimbi ya mawasiliano na Wizara ya Teknohama kuhakikisha mradi huu umeiletea Kenya matumaini ya kustawi kiteknolojia.

Kila sekta kwa sasa inashuhudia madabiliko ya kipekee yanayoletwa na teknolojia, na Kenya inahitaji kujiandaa vilivyo ili kuwa katika mstari wa mbele Afrika katika utoaji wa huduma za kidijitali.

Ulimwenguni kote, huduma nyingi zinazidi kurahisishwa na teknolojia huku mifumo ya zamani ikitupiliwa mbali.

Hivyo, kwa kizazi chetu cha baadaye kunufaika na uvumbuzi wa kiteknolojia kwenye uchumi, tunafaa kuanza kuwafundisha watoto masuala haya. Tunapobahatika kupata ufadhili wa mashirika kama Unicef na Nokia, basi hatuna budi kuyapiga jeki.