Habari Mseto

Wanawake wajidunge sindano wenyewe kuzuia mimba – WHO

July 2nd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na VALENTINE OBARA

WANAWAKE waliohitimisha umri wa uzazi wataweza kujidunga sindano za dawa kuzuia ujauzito iwapo pendekezo la Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), litakumbatiwa.

Kwenye mwongozo mpya kuhusu mbinu za kujitunza kiafya katika ngono na uzazi, WHO inasema pendekezo hilo ni miongoni mwa mengine ambayo yatasaidia kuepusha madhara ya kiafya na kijamii yanayoshuhudiwa hivi sasa katika masuala ya uzazi kimataifa.

Mwongozo huo uliotolewa mwishoni mwa wiki iliyopita umechapishwa wakati ambapo kuna mvutano nchini kuhusu jinsi ya kuepusha mimba za utotoni zinazotatiza wasichana ambao hawajakamilisha masomo ya msingi.

“Dawa za kuzuia mimba zinazoweza kutumiwa na watu kwa kujidunga wenyewe sindano zinafaa ziwepo kama njia zaidi ya kuwezesha watu waliofikisha umri wa uzazi kupokea huduma za kuzuia mimba kwa njia ya kudungwa sindano,” mwongozo huo unasema.

WHO iliongeza kupendekeza dawa za tembe zinazouzwa madukani ambazo kwa kawaida huhitaji ushauri wa daktari, zinafaa kupatikana bila mtu anayetumia dawa hizo kuhitajika kuonyesha muuzaji ana idhini ya daktari.

Kuhusu kukabiliana na maradhi ya zinaa, shirika hilo lilipendekeza mataifa yawezeshe watu kujikusanyia chembe za mwili zinazohitajika kupima iwapo wanaugua maradhi kama vile kisonono na kaswende.

Hii huenda ikawa ni njia ya kuhimiza watu kutafuta matibabu kwani wengi huona aibu kwa sababu ya jinsi ukusanyaji wa chembe za mwili hufanywa.

Kufikia sasa, hatua kubwa zimepigwa katika kupambana na maambukizo ya virusi vya HIV vinavyosababisha Ukimwi lakini inahofiwa uambukizaji wa maradhi mengine ya zinaa unazidi.

Hivi majuzi, wataalamu wa afya walisema hatua kama vile utumiaji wa dawa za kuzuia maambukizo ya HIV baada ya ngono zimefanya watu hasa vijana kupuuza utumiaji wa mbinu tofauti za kuzuia maambukizo ya zinaa.

Kutokana na hali hii, ilielezwa kuwa huenda kuna mafanikio katika kupunguza uambukuzaji wa HIV lakini maradhi kama vile kisonono na kaswende yanaenea kwa kasi kwani dawa zinazotumiwa hazizuii maambukizo ya maradhi hayo.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus alisema mbinu zilizo kwenye mwongozo huo zinalenga kuwapa watu nafasi ya kupokea haki zao za kiafya.

“Wakati watu wanapopewa uwezo wa kujitegemea, wanaweza kuamua na kutekeleza maamuzi kuhusu maisha yao, ikiwemo kuhusu afya ya ngono na uzazi,” akasema kwenye taarifa.