Tumieni mitandao kukuza mapato, serikali yaambia wafanyabiashara
NA MARY WANGARI
SERIKALI Jumatano imewahimiza wafanyabiashara kutumia mitandao ya kijamii kama vile Facebook na Twitter ili kupunguza gharama na kuongeza mapato.
Akizungumza katika hoteli ya Serena, Nairobi, Waziri wa Teknohama, Bw Joe Mucheru alisema matumizi ya mitandao ya kijamii yanaweza kuwasaidia wamiliki wa biashara ndogo ndogo (SMEs) kutangamana na kuongeza idadi ya wateja wao pamoja na kuingiza bidhaa na huduma mpya sokoni.
“Mitandao ya kijamii husaidia kukidhi mahitaji ya wateja popote waliupo kwa njia itakayonufaisha pakubwa uhusiano kati ya mteja na shirika,”alisema
“Vilevile, matumizi ya mbinu kadha za mawasiliano kama vile SMS, barua meme na nyinginezo yanaweza kurahisisha mawasiliano na utangamano kati ya wafanyabiashara wateja.
Aidha, Waziri aliwataka wafanyibiashara nchini kushirikisha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) ili kuinua kiwango cha utendakazi pamoja na ubora wa bidhaa.
Alisema lilikuwa jambo la kutamausha kwamba idadi kubwa ya wamiliki wa SMEs wanatumia mifumo ya kawaida ambayo ina matokeo duni na haiwezi kutegemewa.
“Kutokana na matokeo ya utafiti uliowasilishwa hii leo, ni asilimia 10 pekee ya SMEs katika sekta ya uzalishaji inayotumia teknohama kikamilifu,” alisema.
“Hatuwezi kupuuza kwamba bidhaa zenye kiwango cha juu cha ubora zina ushindani mkubwa kwenye soko. Hivyo basi pana haja ya dharura ya kuingilia kati katika sekta hii kwa kuwa SMEs ndizo nguzo za uchumi wetu,” alisema Bw Mucheru katika hafla ya kuzindua ripoti kuhusu Hali ya Sekta ya Uzalishaji Kenya kufuatia utafiti uliofanywa na shirika la SYPROS kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Strathmore.
Alisema serikali imetenga kitengo mahsusi katika Mpango wa Dijitali kuhusu Uchumi, cha biashara kidijitali pamoja na kuendeleza soko imara la kidijitali linalohusisha kuongeza ubora wa ujumuishaji kifedha, ushindani unaofaa, miundo msingi imara ya data, mifumo bora ya kuwalinda wateja na utangamano wa eneo lote kwa jumla.
Alisema katika kitengo hiki, serikali inatilia maanani biashara kidijitali, huduma za kiifedha kidijitali, pamoja na maudhui kidijitali.
Aidha, alifafanua kwamba serikali ililenga kubuni uchumi wa kidijitali ambapo kila mwananchi na biashara zinaweza kuuza bidhaa halisi, bidhaa na huduma za habari ikiwemo utendakazi bila vikwazo vyovyote.
“Ningependa kuwahakikishia kwamba serikali ni mshiriki mkuu wa jumuia na uchumi kidijitali na tunahisi kwamba ICT ina uwezo wa kubadilisha pakubwa miundo ya maendeleo ya SMEs kwa kupanua nafasi za biashara,”
“Kwa mfano matumizi ya teknolojia kama vile mauzo na matangazo ya biashara mitandaoni itapunguza pakubwa gharama ya uzalishaji na kuongeza uwezekano wa kukuza mapato na faida kwa jumla,”alisema.