• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Tafadhali punguza kasi ya utekelezaji mtaala mpya, Magoha aombwa

Tafadhali punguza kasi ya utekelezaji mtaala mpya, Magoha aombwa

Na VITALIS KIMUTAI

WAZIRI wa Elimu George Magoha amehimzwa kushauriana kwa mapana na wadau kuhusu utekelezaji wa mtaala mpya badala ya kuulazimishia wanafunzi na wadau wengine.

Kiongozi wa Chama Cha Mashinani (CCM) Isaac Ruto, Naibu Gavana wa Bomet Hillary Barchok na Katibu wa Chama cha Kitaifa cha Walimu (KNUT) tawi la Bomet, Malel Langat walisema waziri anapasa kupunguza kasi ili kuzuia kusambaratisha sekta ya elimu.

“Inafaa kuwe na mashauriano ya kina kutoka kwa wizara ya elimu kushirikisha umma badala ya kulazimisha mtaala kwa wadau wa sekta hii,” akasema Bw Ruto.

Akizungumza wakati wa mkutano katika eneo la Ndanai, Kaunti Ndogo ya Sotik, Bw Ruto alisema, “Ni muhimu kama nchi tulinde ubora na viwango vya elimu yetu ambayo imesaidia wataalamu wengi waliofuzu kutoka taasisi mbalimbali kukubaliwa kimataifa.”

Aliongeza: “Yamkini waziri hajali kutokana na jinsi anavyotumia kifua kutekeleza mtaala mpya hata wakati kuna wasiwasi miongoni mwa wadau.”

Alimkosoa pia waziri kwa mipango ya kuwasilisha majina ya wanaoshindwa kulipa karo za shule na taasisi za elimu ya juu kwa taasisi za kuweka rekodi za waliokosa kulipa madeni (Credit Reference Bureau) akisema ni sawa na kuwaadhibu walio masikini na wenye mahitaji katika jamii.

“Wakati utawala wa Rais Uhuru Kenyatta unatekeleza mfumo wa kuwezesha wanafunzi wote wanaokamilisha shule za msingi kujiunga na shule za upili, na vilevile kuboresha taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu, inawezekanaje waziri kuwazia hata kuwasilisha majina ya wanaoshindwa kulipa karo kwa CRB,” akashangaa Bw Ruto.

Kwa upande mwingine, Dkt Barchok alisema kuna hatari mtaala mpya kutofanikiwa kuboresha elimu sawa na jinsi 8-4-4 ilivyolemewa. “Ni vyema tuepuke changamoto ambazo zilikumba mfumo wa 8-4-4 ambao ulikuwa mzuri lakini ukatekelezwa vibaya. Mfumo huo ulivurugwa kila mwaka na hatimaye ukalemewa kabisa kwa sababu ya utekelezaji mbaya,” akasema.

Aliendelea kusema, “Lazima tujifunze kutoka kwa enzi zilizopita na kuelekea mbele, tushauriane kwa kina kuhusu uundaji na utekelezaji wa mtaala mpya”.

Alikuwa akizungumza hivi majuzi aliposimamia mahafali katika taasisi ya elimu ya kiufundi ya Emkwen iliyo Kaunti Ndogo ya Bomet ya Kati.

Alikuwa ameandamana na Afisa Mkuu wa Elimu katika Kaunti, Bw Simon Langat na Diwani wa Silibwet/Township, Bw Haroun Kirui miongoni mwa wengine.

Prof Magoha amekuwa akizozana na KNUT inayoongozwa na Katibu Mkuu Wilson Sossion kuhusu utekelezaji wa mfumo wa 2-6-3-3-3 utakaochukua mahali pa 8-4-4 ambao umetumika kwa miaka 34.

You can share this post!

Njagua aonja uhuru baada ya siku 6 seli

Genge la Gaza lavamia na kuhangaisha Tana River

adminleo