Wafanyabiashara Thika walalama makahaba wamekuwa kero
Na LAWRENCE ONGARO
UKAHABA unazidi kuenea mjini Thika huku wafanyabiashara wakidai umekuwa ni kero kubwa kwa biashara zao.
Bw Shardrack Kitoo ambaye ni mfanyabiashara kwenye barabara ya Uhuru Street mjini Thika, anasema biashara ya ukahaba inaendeshwa hata mchana.
“Tabia hiyo ya ukahaba inaendeshwa hata mchana hadharani na ni aibu kubwa kwetu na kwa wananchi kwa jumla. Cha kushangaza ni kwamba hata wao hutoza wanaume kiwango cha Sh100 kushiriki ngono nao,” alisema Bw Kitoo mnamo Jumatano.
Alisema ifikapo usiku, hapo ndipo ngoma huanza kwa sababu hata tabia ya kupora wapitanjia hushuhudiwa mara nyingi.
“Iwapo utalalamika kwao nao watatoa vijisababu kuwa umekataa kuwalipa haki yao. Hayo ndiyo masaibu wanaume wengi hupitia bila kutarajia,” alisema Bw Kitoo.
Alisema jambo hilo limekuwa ni shida kubwa kwa polisi kwa sababu wanapopelekwa mahakamani polisi anaulizwa na hakimu athibitishe ni jambo lipi linaloonyesha kuwa “huyo aliye kizimbani ni kahaba.”
Bw Daniel Mwangi, ambaye pia ni mfanyabiashara katika mji wa Thika alisema makahaba hao wengi wao huonekana wakizunguka ovyo kando ya maduka za wenyewe huku wakijaribu kuwashawishi wanaume.
“Asubuhi unapopitia kwenye vichochoro vya maduka, utapata vifaa vya kondomu vimetupwa ovyo njiani. Hata watu wengine hujisadia haja kubwa katika maeneo hayo,” alisema Bw Mwangi.
Mwenyekiti wa wafanyabiashara mjini Thika Bw Alfred Wanyoike alisema hawatakubali makahaba hao kuendelea kuwasumbua wenye biashara wakati wanaendesha shughuli zao.
“Sisi kama wafanyabiashara hatutakubali kuyumbishwa na makahaba hao huku tukipata hasara katika biashara zetu,” alisema Bw Wanyoike.
Pendekezo
Alipendekeza waulizie jinsi ya kupata mikopo ya Uwezo Fund ili waendeshe biashara halali badala ya kuuza miili yao kwa wanaume.
Afisa wa polisi mjini Thika Bw Benard Ayoo, alisema tayari wamepata malalamishi hayo na watafanya wawezalo kukabiliana nayo.
Lakini alisema makahaba hao wafikapo mahakamani hujitetea kwa kutaka thibitisho halisi kama kweli wao ni makahaba.
“Kwa hivyo, inafanya hakimu anawatoza faini pekee kwa sababu hakuna thibitisho kamili kuhusu makosa hayo. Kaunti ya Kiambu inastahili kutunga sheria maalumu kuhusu maswala hayo ya ukahaba,” alisema Bw Oyoo.