Habari Mseto

Ruhusa yatoka magunia 12m ya mahindi yaagizwe

July 6th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na BENSON MATHEKA na BARNABAS BII

SERIKALI inapanga kuzipa kampuni za kibinafsi leseni za kuagiza magunia milioni 12.5 ya mahindi bila kulipa ushuru ili kukidhi uhaba uliosababisha bei ya unga kupanda.

Hatua hii inajiri chini ya mwaka mmoja baada ya serikali kukataa kununua mahindi yote ambayo wakulima waliwasilisha katika maghala ya bodi ya nafaka na mazao nchini (NCPB).

Kulingana na waziri msaidizi wa wizara ya kilimo, Andrew Turmur, serikali imeamua kuagiza mahindi kutoka nje kwa sababu yaliyo nchini yatamalizika mwezi wa Julai.

Mwenyekiti wa Maghala Spesheli ya Kuhifadhi Nafaka (SGR), Dkt Noah Wekesa, anasema kuwa kuna magunia milioni 1.5 ya mahindi ambayo wananuia kutoa kwa kampuni za kusaga unga nchini mwezi huu.

Hata hivyo, anasema SGR itatoa mahindi hayo iwapo serikali itaikinga dhidi ya hasara iliyopata baada ya kuuzia kampuni za kusaga unga wa mahindi kwa bei ya Sh2, 300 iliyoagizwa na serikali katika juhudi za kupunguza bei ya unga huo.

Hasara

Kulingana na Dkt Wekesa, serikali inapaswa kukinga SGR dhidi ya hasara iliyopata kabla ya kuagiza mahindi kutoka nje.

Anasema walipoagizwa kuuza gunia la mahindi kwa Sh2,300, bei ya kawaida ilikuwa Sh3,000 kwa gunia la kilo 90.

“Serikali inapaswa kuwajibikia hasara tuliyopata ikizingatiwa kuwa tuliuza gunia la kilo 90 kwa Sh2,300 ilhali bei wakati huo ilikuwa zaidi ya Sh3,000,” alisema Dkt Wekesa.

Alisema kampuni za kusaga unga zimemaliza magunia zilizouziwa na hii imefanya bei ya unga kupanda hadi zadi ya Sh125 kwa pakiti ya kilo mbili.

Mnamo 2017, serikali ilitumia Sh6 bilioni kuagiza mahindi kutoka nje ya nchi ili kupunguza bei ya unga kutoka Sh153 hadi Sh90 kwa pakiti ya kilo mbili.